Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Ulaya zimedhoofisha msimamo wao katika mchakato wa kidiplomasia unaolenga kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran na kwa hiyo watakuwa nafasi “hafifu” katika mazungumzo yoyote yatakayofanyika siku za usoni.

Abbas Araghchi aliyasema hayo Jumapili, wiki moja baada ya kukamilishwa kile kinachoitwa mchakato wa ‘snapback’ ulioanzishwa na Uingereza, Ujerumani, na Ufaransa (zinazojulikana kwa pamoja kama E3) unaolenga kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na mabalozi, mabalozi wadogo na wakuu wa kidiplomasia wa kigeni na wa asasi za kimataifa waliopo katika mji mkuu Tehran, Araghchi alisema, mataifa hayo matatu ya Ulaya yameuchukulia utekelezaji wa ‘snapback’ kama wenzo mpya wa kuiwekea mashinikizo Iran, lakini sasa wameshaona kwamba uanzishaji wa utaratibu huo haujasuluhisha matatizo yoyote bali umeifanya diplomasia iwe tata na ngumu zaidi.

“Diplomasia haina mwisho; ipo siku zote. Lakini suali ni iendelee chini ya masharti gani, ifanyike na pande gani, na kwa kuzingatia uwiano na mlingano gani. Hali ya sasa ni tofauti kabisa na ya zamani,” amebainisha mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.

Araghchi amefafanua kwa kusema: “nchi tatu za Ulaya zimedhoofisha kwa uwazi kabisa msimamo wao katika mchakato wa kidiplomasia na kwa kiasi kikubwa zimepoteza mantiki ya kufanya mazungumzo nao. Katika azimio lolote linalotarajiwa kwa ajili ya mazungumzo, nafasi ya Ulaya itapungua zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.”

Itakumbukwa kuwa, mnamo Agosti 28, nchi tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinazounda Troika ya Ulaya zilitumia utaratibu wa ‘snapback’, mchakato wa siku 30 ulioainishwa katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 – ambayo yalitelekezwa na Marekani- na kurejesha vikwazo vyote vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Tehran ilipinga hatua hiyo na kusema kuwa ni kinyume cha sheria, ikitolea mfano hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA mwaka 2018 na uamuzi wa nchi tatu za Ulaya wa kufungamana na vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vilivyowekwa na Washington dhidi ya Iran, badala ya kutekeleza majukumu yao katika JCPOA.

Sambamba na hayo, juhudi zilizofanywa hivi karibuni na Russia na China zilizolenga kuipa diplomasia muda zaidi wa kutatua mzozo wa mpango wa nyuklia wa Iran hazikuweza kupata kura za kutosha katika Baraza la Usalama mnamo Septemba 26.

Siku mbili baadaye, Marekani na nchi za Ulaya zilidai kuwa maazimio ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na vikwazo vinavyohusiana na maazimio hayo vimerejshwa tena, na kuzitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitekeleze hatua za vikwazo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *