Maandamano makubwa ya wananchi wa mataifa ya Ulaya dhidi ya sera za utawala wa kizayuni wa Israel huko Ghaza yangali yanaendelea.

Licha ya kupendekezwa makubaliano ya usitishaji vita huko Ghaza yaanze kutekelezwa katika siku zijazo, hasira na chuki dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika eneo hilo la Palestina uliloliwekea mzingiro zingali zinaendelea kuonyeshwa kimataifa. Kuhusiana na hilo, maelfu ya waandamanaji katika nchi mbalimbali za Ulaya ikiwemo Ufaransa na Uhispania wametaka kukomeshwa uungaji mkono wa kijeshi wa nchi zao kwa Tel Aviv.

Maandamano hayo sasa yamegeuka kuwa moja ya mavuguvugu makubwa zaidi ya umma katika bara la Ulaya, na kuonekana kuwa ni kiashiria cha mabadiliko ya kimsingi katika mtazamo wa wananchi wengi wa nchi za bara hilo kuhusiana na sera za Israel katika vita vya Ghaza.

Kuhusiana na hilo, katika siku za hivi karibuni, maelfu ya raia wa Ulaya katika nchi mbalimbali zikiwemo Italia, Ureno, Uhispania, Ufaransa na Uingereza wameshiriki katika maandamano makubwa ya umma wakizitaka serikali zao ziache kuisaidia na kuiunga mkono kijeshi na kisiasa Israel na badala yake zichukue misimamo madhubuti zaidi dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu. Maandamano hayo yaliyoenea kila mahala yanaonyesha mabadiliko makubwa yaliyojitokeza katika mtazamo wa watu wa Ulaya kuhusiana na kadhia ya Palestina na uchokozi uliofanywa na Israel, na ni kielelezo cha kuongezeka uelewa na kuguswa mno wananchi wa Ulaya na jinai zinazofanywa na Israel huko Ghaza.

Japokuwa ukubwa wa jinai za Israel, kutoheshimu utawala huo wa kizayuni sheria zozote za kibinadamu au za kimataifa, na kuakisiwa katika vyombo vya habari baadhi ya jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina wanaoishi Ghaza ni miongoni mwa sababu zilizoyafanya maoni ya umma barani Ulaya yashughulishwe na jinai hizo zinazofanywa na jeshi la kizayuni na kutaka zikomeshwe, lakini sababu kuu za kufanyika maandamano hayo zinaweza kutajwa kuwa ni hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa Ghaza, wasiwasi walionao watu kutokana na sera zinazoendelea kutekelezwa na Israel hususan za mauaji ya kimbari, na kufanya juhudi za kutoa mashinikizo kimataifa ya kumaliza vita vya Ghaza.

Hali mbaya ya kibinadamu imeshtadi katika Ukanda wa Ghaza kufuatia vita vya kikatili vilivyoanzishwa na Israel hasahasa katika miezi ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, zaidi ya Wapalestina 67,000 wameuawa shahidi na maelfu wamejeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel. Hii ni katika hali ambayo hospitali nyingi na vituo vya matibabu katika eneo hilo vimebomolewa kikamilifu; na uhaba wa madaktari, dawa na vifaa vya tiba unahisika waziwazi. Kwa upande mwingine, vivuko vya kuingia na kutoka Ghaza vimefungwa na utawala ghasibu wa Israel kwa miezi kadhaa sasa na hakuna uwezekano wowote wa kufikisha misaada kwa wakazi wa eneo hilo. Hali hii imesababisha baa la njaa na vifo kwa Wapalestina wengi wanaoishi Ghaza, hususan watoto wadogo. Hali hiyo ya maafa na hasahasa msimamo wa kuishadidisha unaoshupaliwa na viongozi wa utawala wa Kizayuni, vimeziumiza hisia za walimwengu na kuibua wimbi kubwa la maandamano ya umma katika nchi mbalimbali za Ulaya.

Ijapokuwa serikali za Ulaya zimeuunga mkono utawala wa Kizayuni tokea mwanzoni mwa vita vya Ghaza na kuupatia misaada ya kifedha, kisiasa na kijeshi, lakini hivi sasa maoni ya wananchi barani Ulaya yamefikia hadi ya kujihisi ni mshirika wa jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu na yamesimama dhidi ya sera za utawala huo huko Ghaza.

Kuhusiana na suala hili, katika siku za hivi karibuni, maandamano makubwa yamefanyika katika nchi mbalimbali za Ulaya. Kwa mfano mjini Roma, umefanyika mgomo mkubwa zaidi wa umma wa vyama vya wafanyakazi kwa ajili ya kutetea haki za Wapalestina. Katika miji mikubwa ya Uhispania ya Madrid na Barcelona, ​​​​maelfu ya watu wameandamana dhidi ya Israel na kutoa mwito wa kuhitimishwa vita huko Ghaza. Maandamano sawa na hayo yamefanyika pia katika miji ya Lisbon, Ureno na London, Uingereza ambako waandamanaji wametoa nara na kaulimbiu za haki za binadamu wakitaka kukomeshwa mauaji ya Wapalestina na kuzishinikiza serikali zao zibadilishe misimamo yao.

Kusema kweli wananchi wa Ulaya wamechoshwa na ufichaji wa jinai za Israel uliokuwa ukifanywa na serikali zao, na sasa wanataka vita dhidi ya Ghaza vihitimishwe na jinai zinazofanywa na Wazayuni zikomeshwe.

Kuhusiana na hilo, baadhi ya serikali za nchi kama, Ufaransa, Uingereza,  Australia, Canada, Ureno, Ubelgiji, Luxembourg, Andorra, Malta na Monaco, zilitangaza hivi karibuni kuitambua Palestina kuwa ni nchi huru katika uga wa kimataifa zikiungana na nyingine 147 ambazo zimeshatangulia kufanya hivyo. 

Kwa ujumla, tunaweza kusema kwamba, maandamano ya kupinga sera za kichokozi na kivamizi za utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina sasa yamegeuka kuwa harakati na vuguvugu la kimataifa ambalo lengo lake ni kubadilisha sera za kimataifa kuhusiana na mgogoro wa Palestina na kuhitimisha vita vya Ghaza. Vuguvugu hilo la umma sasa limekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali za Magharibi. Lakini pamoja na hayo, kinachoonekana kwa uwazi ni sera za kiundumakuwili zinazofuatwa na nchi za Ulaya ambazo zingali zinaendelea kivitendo kuunga mkono sera za Israel. Mgongano huu wa wazi katika sera za serikali za Ulaya sio tu unatilia shaka uhalali wa kisiasa wa serikali za Magharibi, lakini pia unaonyesha pengo kubwa lililopo kati ya vinara wa kisiasa na wananchi wao, ambao hawawezi tena kuvumilia dhulma zinazotetewa na serikali zao…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *