Karibuni wasikilizaji wapendwa kutegea sikio kipindi hiki cha makala ya wiki tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah, kuweni nami hadi tamati.

Sayyid Hassan Nasrullah mujahid huyo mkubwa alikuwa utajiri na tunu adhimu si tu kwa ajili ya Lebanon bali pia kwa ajili ya Ulimwengu wa Kiislamu. Utajiri ambao ungali unashuhudiwa hadi sasa. Sayyid Hassan Nasrullah ametuacha lakini utajiri alioutengeneza umebaki hadi hii leo. Alikuwa na umri wa miaka 15 tu alipoelekea Najaf na kukutana na Imam Musa al-Sadr. Tangu mwanzoni walipofahamiana, alikuwa na hamu kubwa na ya kushangaza kuhusu Imam Sadr na alikuwa na wasiwasi kila wakati kwamba anaweza kuuawa. Alikuwa na umri wa miaka 17 alipoota ndoto ya ajabu. Yeye mwenyewe anasimulia kwamba usiku huo sikuwa nikimfikiria kabisa Imam Musa al-Sadr, bali aliota kuwa Imam Musa aliwaalika watu kwenye sherehe kubwa. Sayyid Hassan alipofika mahali mkutano ulipokuwa ukifanyika, alimuona Imam Musa amekaa ndani ya chumba kikongwe katikati ya jangwa kubwa pasina mavazi yake ya kidini. Kulikuwa na watu wachache katika chumba hicho, jambo ambalo lilimshangaza Sayyid Hassan kwa sababu siku zote marasimu ya Imam Musa huhudhuriwa na watu wengi. Hali hiyo ya wasiwasi ya siku zote ilimjia tena kwa mara ya pili ndotoni; isije ikawa kuna mtu anapanga kumuua Imam Musa!!

Sauti ya adhana ilisikika. Imam alisimama kuswali. Watu waliokuwa wakijiandaa kuswali nyuma yake ghafla walimuona mwanaume mrefu aliyeshika upanga akielekea kwa Imam. Sayyid Hassan kisha akamwendea Imam Musa na kumkinga na mtu huyo.

Watu wote walisimama kuswali lakini ghafla ilisika sauti ikisema Imam Musa Sadr ameuawa. Swala haikumalizika, Sayyid Hassan akamkamata mtekeleza shambulizi karibu na mlango wa kutoka chumbani na akamuangusha chini kwa upanga ule ule aliompigia Imam.  

Sayyid Hassan alimsimulia ndoto yake hiyo Sheikh wa Kiiraqi mweledi wa masuala ya irfani na utabiri wa ndoto  na akaifasiri ndoto yake kama ifuatavyo: Siku moja Imam Musa al-Sadr atauawa kwa dhulma na akiwa peke yake; na atazikwa mahali fulani jangwani, na kaburi lake halitajulikana. Siku moja wewe utawakuwa mrithi na kuendeleza njia yake na malengo yake yatatimizwa kupitia wewe. Ndoto hii kwa hakika ilikuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu alikuwa amemchagua Sayyid Hassan kutekeleza majukumu makubwa. Ilichukua muda wa miaka minne kwa ahadi hii ya Kimungu kutimia. Mwaka mmoja baada ya ndoto hii, Imam Musa Sadr alikwenda Libya na hakurejea tena. Miaka mitatu baada ya Imam Musa Sadr kutoweka, Sayyid Hassan Nasrallah, akiwa na umri wa miaka 21 tu, akawa Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa amri ya Imam Ruhulah Khomeini (M.A).

Nasrullah hakuwahi kulala usingizi mnono hata usiku mmoja katika kipindi cha miaka 32 ya uongozi wake. Alipigana katika medani mbili za vita tangu mwanzoni mwa ujana wake. Vita moja alipigana ndani na nyingine nje ya nchi. Ndani ya Lebanon, yeye na wafuasi wake walikabiliana na wapinzani ambao, kwa upande mmoja, kwa kujua au kinyume chake walichochea moto wa hitilafu za kidini na kuifanya nchi hiyo kuwa uwanja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kwa upande mwingine, kwa kusisitiza juu ya suala la kuipokonya silaha Hizbullah, walikuwa wakisonga mbele ili kufanikisha malengo ya utawala wa Kizayuni ya kuwafanya wananchi  madhulumu wa Lebanon kushindwa kujihami. Katika medani ya nje pia Nasrullah alikabiliana na adui Mzayuni. Adui ambaye kutokubali kwake kushindwa kulizilazimisha nchi zote za Kiarabu kurudi nyuma mkabala wa matakwa yake ya kidhalimu.

Kwa miaka mingi, eneo la kusini mwa Lebanon limekuwa likiungua chini ya buti za wavamizi maghasibu wa Kizayuni. Tangu mwaka 1982, vifaru vya Israel vimekuwa vikizunguka katika ardhi ya Lebanon na utawala huo umeasisi kwa ajili yake eneo kusini mwa nchi hiyo kwa jina la “Ukanda wa usalama.” Wakazi wa kusini mwa Lebanon kila uchao walikuwa wakihisi juu yao kivuli cha askari ajinabi na kukabiliwa na milipuko ya mabomu, kubomolewa nyumba zao na kutiwa nguvuni. Ukanda wa usalama wa Wazayuni ulikuwa ukanda wa mauti na utumwa kwa wananchi wa Lebanon.

Katikati ya miaka hiyo migumu, vijana wa Hizbullah waliinuka na kuanzisha vita vipya. Hawakuwa na jeshi lenye silaha na lililopangika vizuri lakini walikwenda kukabiliana na adui wakiwa na imani na azma thabiti iliochipuka kutoka kwenye udongo na damu. Operesheni za kushtukiza, kujitoa muhanga, ufyatuaji risasi wa kushtukiza wa wanamuqawama vilikuwa jinamizi kwa Wazayuni maghasibu. Mapigano yaliendelea kwa miaka kadhaa hadi pale ngano inayosema kuwa “jeshi lisiloshindwa la Israel” ilipofutiliwa mbali kabisa. Hatimaye usiku wa tarehe 25 Mei mwaka 2000, jeshi la Israel lilikimbia Lebanon katika kimya cha kutisha. Bila ya mazungumzo, bila makubaliano ya amani na bila hata sharti moja. Kilichokuwa kimesalia ni bendera za ushindi wa Hizbullah na sauti kuu ya Nasrallah iliyokuwa ikisema: “Nyinyi mumeshinda… kwa damu ya mashahidi, kwa subira ya akina mama, kwa imani na istiqama”.

MUZIKI                                                                          MUZIKI

Ushindi huo mpya ulikuwa mwanzo tu wa njia, mwanzo wa kuibuka muqawama wa Kiislamu katika eneo. Kushindwa kwa fedheha Wazayuni katika vita vya siku 33 mwaka 2006 ilikuwa hatua iliyofuata ya Nasrallah kwa ajili ya kuwalinda wananchi wa Lebanon. Wananchi Washia wa Lebanon, Wasuni, Wakristo na Wadruzi, wote walifurahishwa na kipigo alichokipata adui na walikuwa wameziunganisha nyoyo zao kutokana na  mapenzi yao kwa Hizbullah na Nasrallah. Umoja na mshikamano vilichukua nafasi ya mgawanyiko na hitilafu, na Lebanon ikawa imepata amani ya kudumu baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Amani na umoja huo ulimtia hofu adui Mzayuni; na yote haya yaliwezekana chini ya uongozi wa Nasrallah. Ushindi wa watu wa Lebanon ukawa mwanga kwa watu wa Palestina, Iraq na wapigania uhuru wote katika eneo.

Baada ya mafanikio na ushindi wa Hizbullah mwaka 2000 ambapo muqawama wa Palestina pia uliibuka na ushindi mkubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni katika vya siku 22, siku 8, siku 51 na siku 12 miongoni mwa ushindi wote huo ulioupata muqawama wa Palestina, vita vya siku 12 vinavyojulikana kwa jina la “Upanga wa Quds”, ndivyo mashuhuri zaidi. Cheche ya awali ya vita hivyo ilichochechewa na hatua ya wanajeshi wa  Israel ya kuvamia maeneo mbalimbali ya Msikiti wa Al-Aqsa na kufuatia walowezi wa Kizayuni kunajisi matukufu ya Waislamu.

Tarehe 10 Mei mwaka 2021 inayosadifiana na Ramadhani 25 mwaka 1442 Hijria Brigedi za Shahidi Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Hamas zilitoa taarifa ambapo ziliupatia utawala wa Kizayuni muda wa hadi kufikia saa kumi na mbili jioni uwe umekomesha uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al Aqsa. Muhammad al Dhaif Kamanda mtajika wa Brigedi za Izzuddin Qassam aliuonya utawala wa Kizayuni kupitia filamu fupi na kusema: “Zama za kutochukua hatua na kuadhibu zimekwisha.” Vita vya pande zote kati ya pande mbili vilianza baada ya kumalizika muhula wa Hamas kwa utawala wa Kizayuni. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kuwahi kushuhudiwa muqawama wa Palestina ukianzisha vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Muqawama wa Palestina sambamba na kuanza mashambulizi kati yake na utawala wa Kizayuni ulitangaza kuwa: ‘Kuanzia sasa kila Mpalestina, popote alipo huko Palestina anaungwa mkono na muqawama, na kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya Wapalestina na maeneo matakatifu ya Waislamu yatakabiliwa na jibu la muqawama.’

Ubunifu huu wa muqawama ulipulizia mwanga wa matumaini ndani ya mioyo ya Wapalestina, na kuwafanya watangaze katika kila nukta mshikamano wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina, ambapo mkundi ya Wapalestina kuanzia Lebanon, Jordan hadi Syria yalipambana vilivyo na wazayuni maghasibu. Mapigano madogo polepole yakageuka kuwa vita halisi. Muqawama ulipodhihirisha uwezo wake katika uwanja wa vita, utawala wa Kizayuni ulilazimika kutoa wito wa kusitishwa mapigano. Wazayuni walikubali masharti yote ya muqawama na kuafiki kukomesha uvamizi wa walowezi na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa.

MUZIKI                                                                                   MUZIKI

Hassan Nasrullah alikuwa kiongozi wa aina yake ambaye mbali na Palestina alihami na kuzitetea nchi nyingine za Kiarabu mbele ya njama na uvamizi wa adui Mzayuni na Marekani. Huko Iraq, Hizbullah haikuingia moja kwa moja kwenye uwanja wa vita, lakini ilianzisha uhusiano wa kifikra, kitaasisi na kimafunzo kati ya  wanamuqawama wa Iraq na Hizbullah. Mafunzo ya kijeshi na uzoefu wa kivita wa Hizbullah kusini mwa Lebanon na uzoefu wa mapigano huko kusini mwa Lebanon ulihamishiwa kwa Mujahidina wa Iraq na hivyo kuandaa uwanja wa kudhihiri mbegu kuu za muqawama dhidi ya maghasibu.

Wakati wa mgogoro wa ugaidi dhidi ya Syria mwaka 2011 na vita vikubwa vya kimataifa vilivyoanzishwa na Marekani dhidi ya wananchi wa Syria; Hizbullah ikiongozwa na shahidi Sayyid Hassan Nasrallah ilikuwa miongoni mwa makundi ya kwanza ya mhimili wa muqawama kutoa idadi kubwa ya vijana wake bora na makamanda kwa ajili ya kulinda mamlaka na kuwahami wananchi wa Syria.

Mwaka 2015, wakati karibu Ulimwengu wote wa Kiarabu ulipoungana dhidi ya Yemen, Sayyid Hassan alisisitiza katika hotuba yake ya kwanza kuhusu vita vya Yemen kwamba uvamizi dhidi ya Yemen ulikuwa umefanyika katika fremu ya mpango wa kina na mkubwa kwa lengo la kubadili ramani ya Mashariki ya Kati kwa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. Alitambua vyema kwamba Wayemeni ni nembo ya muqawama na kwamba wangesimama imara kukabiliana na njama za mhimili wa Marekani na Uzayuni katika siku zijazo. Kwa utaratibu huu, Sayyid shahidi wa muqawama alikuwa akiitaja kadhia ya Yemen kuwa ni vita vya kuainisha hatima ambapo mhimili wote wa muqawama ulikuwa na wajibu wa kuiunga mkono nchi hiyo. Matokeo ya uungaji mkono huo tunayashuhudia sote hii leo kupitia himaya na uungaji mkono usio na kifani wa Wayemeni kwa Gaza inayodhulumika.

Licha ya utendaji huu wa kijasiri na wa kimataifa, imebainika wazi kikamilifu ni kwa nini adui Mzayuni alikuwa akimuoga kiasi hicho kiongozi wa muqawama. Wazayuni kwa miaka mingi walipanga njama ya kumuua kigaidi, na katika kila vita walijaribu kumuondoa katika njia yao. Hasa mwaka mmoja uliopita, tukio la kutisha lilijiri katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.

Tani kadhaa za mabomu yenye kusababisha uharibifu mkubwa yalitua kwenye jengo moja tu, jengo ambalo lilikuwa makao makuu ya Hizbullah huko Lebanon. Mabomu hayo yaliharibu jengo hilo na kupasua ardhi chini yake katika umbali wa mita 70 hata hivyo hayakufika katika mwili wa kiongozi huyo shupavu. Baada ya shambulio hilo la kikatili lililodhihirisha kiwango cha uadui na chuki za Wazayuni dhidi ya kiongozi huyo wa muqawama, wafanyakazi shujaa wa huduma za uokoaji walimtafuta kwa masaa kadhaa Sayyid Hassan Nasrullah. Hatimaye, waliupata mwili wake ukiwa mzima. Alikuwa ameaga dunia kwa kukosa hewa ya oksijeni au kuvuta pumzi ya gesi zenye sumu. Huyo ndiye Sayyid Hassan Nasrullah mujahid mkubwa ambaye alikuwa tunu adhimu si tu kwa ajili ya Lebanon bali pia kwa ajili ya Ulimwengu wa Kiislamu. Utajiri ambao ungali unashuhudiwa hadi leo.

MUZIKI                                                                                        MUZIKI 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *