BAADA ya wiki tatu, Faustin alipelekwa tena mahakamani na mimi nikaendelea na ushahidi wangu ambapo niliieleza mahakama kwamba mshitakiwa amechunguzwa akili yake na amethibitishwa kuwa hakuwa na matatizo ya akili. Nikakitoa cheti cha daktari kilichothibitisha kwamba Faustin alikuwa mzima.

Baada ya kuuelezea uchunguzi huo wa daktari, wakili wa utetezi aliniuliza swali jingine kabisa.

“Katika maelezo yako ya awali ulisema kuwa ulishangaa mshitakiwa alipokiri kwako kuwa amewanyonga watu wanne, je, ulimuuliza ni kwanini alifanya hivyo?”

“Nilimuuliza.”

“Alikwambia ni kwanini aliwanyonga watu hao?”

“Aliniambia kuwa aliwanyonga baada ya kugundua kuwa walitoroshwa jela na afisa wa gereza.”

“Hebu fafanua, hao waliouliwa walikuwa jela?”

“Ndiyo, walikuwa jela kabla ya kutoroshwa na mkuu wa gereza.”

“Walikuwa jela kwa kosa gani?”

“Ngoja nieleze ilivyokuwa…”

“Ndiyo, eleza.”

“Hao watu walishitakiwa kwa kosa la kumuua kijana mmoja ambaye alikuwa ni ndugu na mshitakiwa, wakahukumiwa na mahakama kunyongwa. Wakiwa katika gereza wakisubiri adhabu yao ndipo walipotoroshwa na kurudi uraiani, wakawa wanaishi kama raia wa kawaida. Sasa mshitakiwa aligundua kuwa watu hao wameachiwa kinyemela ndipo alipowasaka na kuwanyonga mmoja mmoja.”

“Kumbe hao watu walishahukumiwa kunyongwa! Sasa kama walishahukumiwa kunyongwa na wamenyongwa na mshitakiwa, kuna kosa gani?”

“Kosa lipo. Yeye hakuwa na mamlaka ya kuwanyonga.”

“Kwani hapa mshitakiwa ameshitakiwa kwa kosa gani?”

“Kosa la mauaji ya kukusudia.”

“Sasa mshitakiwa ana kosa la kujitwalia mamlaka ya kuwanyonga watu waliohukumiwa na mahakama kunyongwa au ana kosa la kuua kwa kukusudia?”

“Anakabiliwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia.”

“Si kosa la kujitwalia mamlaka ya kuwanyonga watu waliohukumiwa kunyongwa?”

“Hapana.”

“Nilikuuliza mwanzo kwamba mshitakiwa amefanya kosa gani wakati watu aliowanyonga walishahukumiwa na mahakama wanyongwe, ukaniambia kosa lipo nalo ni yeye kutokuwa na mamlaka ya kuwanyonga. Sasa kwanini unaniambia kosa lake ni kuua kwa kukusudia? Mshitakiwa anakabiliwa na makosa mangapi hapa?”

Hapa wakili aliuliza kwa msisitizo.

“Kosa moja la kuua kwa kukusudia.”

“Kama hawa watu wameshahukumiwa na mahakama kuwa wanyongwe, yeye ana kosa gani?”

“Ana kosa la kutokuwa na mamlaka ya kuwanyonga.”

“Si kosa la kuua kwa kukusudia?”

Nikaona sasa wakili anazungusha akili yangu. Ananifanya nikiri kile ambacho nimekikana.

Dhamira yake nilishaijua. Alitaka kututia katika makosa kwamba tumemshitaki Faustin kosa la kuua kwa kukusudia wakati tulistahili kumshitaki kwa kosa la kujitwalia mamlaka ya kunyonga watu kinyume cha sheria.

Kwa vile alishanitia kwenye mtego wa kusema kwamba mshitakiwa ana kosa la kujitwalia mamlaka ya kuwanyonga watu, nikaona nisijitie tena kwenye upumbavu wa kukana kitu nilichokisema, nikaamua kunyamaza kimya.

“Twende na swali jingine. Ni kwanini mlichukia wakati aliyepewa mamlaka ya kuwanyonga washitakiwa waliohukumiwa kunyongwa anawaachia, halafu mwananchi mwenye uchungu akatekeleza amri ile?”

“Ni kwa sababu huyo mwananchi hakuwa na mamlaka hayo.”

“Vizuri. Sasa nimeshajua kosa la mshitakiwa si kuua kwa kukusudia bali kosa lake ni kutokuwa na mamlaka ya kunyonga,” wakili huyo akajisemea kama aliyekuwa anasema peke yake.

Sikumjibu kitu kwa sababu hakuniuliza swali.

“Je, mlichukua hatua gani dhidi ya mkuu wa gereza aliyewatorosha wafungwa hao?” wakili wa upande wa utetezi akaniuliza.

Kabla sijajibu swali hilo, wakili wa serikali akasimama na kupinga swali nililoulizwa.

“Mheshimiwa jaji, swali hilo halihusiani na kesi hii. Shahidi wangu hapaswi kulijibu,” akasema.

“Wakili wa utetezi, swali hilo halihusiki na kesi hii,” mheshimiwa jaji akamwambia wakili wa serikali.

Wakili huyo alikubali kuuliza swali jingine.

Lakini halikuwa swali, bali alizusha hoja iliyoishangaza mahakama nzima.

“Je, huoni kwamba mlikosea kumshitaki mshitakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia na kwamba mlipaswa kubadili shitaka hilo?” wakili wa utetezi akaniuliza.

“Mimi siye ninayeandaa mashitaka. Siwezi kuzungumzia hilo.”

“Ninajua, lakini nilitaka maoni yako kama mpelelezi wa kesi hii.”

“Mimi naona shitaka lililopo ni sahihi.”

“Ni sahihi kwa mtu ambaye alitenda kosa la kujitwalia mamlaka ya kunyonga watu waliohukumiwa kunyongwa bila kuwa na mamlaka hayo, halafu ashitakiwe kwa kosa jingine?”

“Yeye aliua, ndiyo maana ameshitakiwa kwa kosa la kuua.”

“Acha haraka, sisi tunazungumzia uhalali wa shitaka. Sote tunajua kwamba anadaiwa ameua, lakini aliua watu ambao hawakuwa na uhalali wa kuishi kwa kuwa walishahukumiwa kufa.”

“Sasa yeye hakuwa na mamlaka ya kuwaua.”

“Enhee… umekuja kule kule ninakotaka mimi. Sasa kwanini hamkushitaki kwa kosa hilo la kujitwalia mamlaka asiyokuwa nayo kwa sababu aliowaua walitakiwa kuuawa?”

“Jaji ndiye atakayeamua.”

Wakati wote wakili huyo akinihoji nilikuwa nikijiambia, mawakili wa utetezi wana usumbufu mkubwa wa kulazimisha vile wanavyotaka wao.

Nilikuwa na uhakika kwamba ushahidi wangu alikuwa ameutia matundu mengi kwa lengo la kutaka kuionyesha mahakama kwamba upande wa mashitaka umekosea kumshitaki Faustin kwa kosa la kuua kwa kukusudia kwa vile waliouawa tayari walikuwa wameshahukumiwa kufa.

Sasa mimi niliona tuiachie mahakama iamue.

Nilikuwa nimechoka kusimama na nilitamani wakili huyo amalize maswali yake.

“Nina swali la mwisho,” wakili akaniambia na mimi nikamjibu.

“Uliza.”

“Unajua kwamba upuuzi wa mkuu wa gereza aliyewatorosha wale wafungwa bila kuwanyonga ndio uliosababisha Faustin awanyonge yeye?”

“Ninajua.”

“Na unajua kwamba kosa alilofanya mkuu wa gereza linaweza kusababisha hasira kwa ndugu wa kijana aliyeuawa na watu hao waliotoroshwa?”

“Ndiyo, ninajua.”

“Na unajua kwamba katika hali ya hasira mtu unaweza kukosa subira na kuua?”

“Ninachosisitiza mimi ni kwamba mshitakiwa baada ya kuwaona wale watu alipaswa kuripoti polisi na si kujitwalia mamlaka ya kuwaua.”

“Kwani wangekamatwa si wangeuawa hivyo hivyo?”

“Mimi siwezi kujibu swali hilo,” nikamwambia wakili nikiwa nimekasirika.

“Wewe ni shahidi, unapaswa kujibu maswali yangu.”

“Maswali mengine hayalingani.”

“Eti nini?”

Nikanyamaza kimya.

“Sote tukiamua kukaa kimya, hili shauri litafika mwisho kweli?”

“Niulize swali jingine.”

“Nakuuliza swali hilo hilo. Kama mshitakiwa angetoa ripoti polisi na watu hao wakakamatwa, adhabu yao ingetekelewa au wangeachiwa?”

“Tungewafikisha mahakamani na mahakama ingeamua,” nikamjibu.

“Mahakama ingeamua nini?” wakili akajiuliza baada ya mimi kujibu kinyume na matakwa yake.

“Sijui.”

Wakili alinitupia jicho kali kisha akakaa kwenye kiti. Akamtazama jaji.

“Mheshimiwa, nimemaliza maswali yangu.”

“Shahidi mwingine,” jaji akasema.

Shahidi aliyeitwa baada ya mimi alikuwa Sajini Meja Ibrahim, mtaalamu wa alama za vidole.

Na yeye alitoa ushahidi wake jinsi alivyogundua kwamba alama ya dole iliyokuwa kwenye karatasi zilizokutwa katika shingo za watu walionyongwa zilikuwa alama za Thomas, mtu ambaye aliuawa miaka miwili iliyopita.

Pia alieleza alivyothibitisha kwamba alama hizo zilikuwa za marehemu Thomas baada ya kaburi lake kufukuliwa na kuchukuliwa alama zake.

Kuhusu watu wanne walionyongwa na Faustin, Sajini Meja Ibrahim alieleza kuwa alichukua alama zao za vidole na kugundua kuwa walikuwa ni watu ambao walishitakiwa kwa kosa la mauaji ya Thomas na kuhukumiwa na mahakama kunyongwa.

Baada ya kumaliza maelezo yake, wakili wa utetezi alisimama na kuanza kumhoji maswali.

“Umesema kwamba alama ya dole gumba uliyoiona katika karatasi zilizokutwa katika shingo za watu walionyongwa hazikuwa za mshitakiwa?”

“Ndiyo.”

“Kwanini hii alama ya dole gumba iliwashughulisha polisi?”

“Tulihisi kwamba aliyeweka alama hiyo ndiye aliyewanyonga watu hao.”

“Lakini mlikuja kugundua kuwa si yeye?”

“Tulikuja kugundua kuwa mwenye alama ile naye alikwishauawa. Mshitakiwa alipachika dole la mtu aliyeuawa na kuzikwa ili kuwababaisha polisi.”

“Sasa katika uchunguzi wako wa alama za vidole ni mahali gani uligundua kuwa muuaji alikuwa mshitakiwa?”

“Katika uchunguzi wangu sikugundua jambo hilo.”

“Sasa hapa umekuja kutoa ushahidi gani?”

Sajini Meja alibabaika kujibu swali hilo kabla ya kusema,

“Sijaelewa swali.”

“Wewe ni shahidi wa upande wa mashitaka na ushahidi wako ulitakiwa ulenge kwenye kosa la mshitakiwa, si ndiyo?”

“Ndiyo.”

“Sasa kama unasema kwamba katika uchunguzi wako wa alama za vidole hukugundua kwamba mshitakiwa ndiye aliyewaua hao watu, umekuja kutoa ushahidi wa nini hapa?”

“Mimi nimeitwa nije nitoe ushahidi kuhusu uchunguzi wangu, na ndiyo nimeutoa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *