NAMNA ambavyo mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah anavyoendelea kucheka na nyavu, imewafanya wataalamu wa soka kumuona ni mshambuliaji sahihi wa kikosi hicho ambaye atatoa ushindani mkubwa kwa mastaa wengine wa timu hiyo.
Oktoba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan, wafungaji ni Sowah na Jean Charles Ahoua.
Bao hilo la Sowah, limewafanya mastaa wa zamani kuona kitu kwa Mghana huyo aliyefunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2024-2025 akiwa na Singida Black Stars aliyojiunga nayo Januari 2025 kupitia usajili wa dirisha dogo.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema ujio wa Sowah kwa Wanamsimbazi kutambua ushindani wa namba na kuongeza uimara wa safu ya ushambuliaji.
“Hilo litamsaidia Ahoua aliyekuwa kinara wa mabao (16 na asisti tisa) msimu uliyopita kujituma zaidi akijua kuna mtu mpambanaji kaongezeka kikosini, kitendo cha kila mmoja kufunga bao moja mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal kinaendelea kuchochea bidii baina yao,” amesema Mogella na kuongeza;
“Japokuwa ni mapema aliyetambulishwa kama Menaja Mkuu Simba, Dimitar Pantev namuona ana mpira wa kushambulia ambao ni mfumo wa timu, akipewa muda naamini mambo mazuri yanakuja kwa klabu hiyo.”
Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel, amesema: “Mechi hiyo ya kirafiki inamsaidia Pantev kuendelea kuwasoma wachezaji akisaidiana na Selemani Matola hasa kuona mambo ya kuyafanyia kazi mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs.
“Kocha anaanzia kukipanga kikosi chake katika mazoezi na hizo mechi za kirafiki, muendelezo alionao Sowah katika kufunga mabao ambapo katika mechi za Ligi Kuu tayari kafunga bao moja, hilo linaonyesha ataisaidia sana Simba pia atampa ushindani Ahoua ambaye alikuwa kinara wa mabao msimu uliyopita kuhakikisha anapambana kuwa na muendelezo wa kile alichokifanya.”
Sowah ambaye anapigania nafasi kikosi cha kwanza eneo la ushambuliaji na Seleman Mwalimu na Steven Mukala, amefunga bao moja kwenye ligi dhidi ya Fountain Gate huku akianza katika mechi mbili kati ya tano. Kwa upande wa Mwalimu aliyeanza katika mechi moja, naye ana bao moja alilofunga dhidi ya Namungo. Mukwala bado hajafunga huku akianza katika mechi mbili kati ya tano.