
Umoja wa Mataifa utapunguza idadi ya walinda amani wake duniani kote kwa 25% katika miezi ijayo, au kati ya 13,000 na 14,000 wanajeshi na polisi, kutokana na ukosefu wa fedha, hasa unaohusishwa na Marekani kukata misaada yake, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza siku ya Jumatano, Oktoba 8.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Itabidi tuwarudishe makwao, kupunguza kwa takriban 25% idadi ya askari wetu wa jeshi na polisi wa kulinda amani, pamoja na vifaa vyao, na idadi kubwa ya wafanyakazi wa misheni ya kiraia pia wataathiriwa,” afisa huyo amesema kwa sharti la kutotajwa.
Bajeti ya ulinzi wa amani ya mwaka 2025-2026 (kuanzia mwezi Julai 2025 hadi mwezi Juni 2026) ni takriban dola bilioni 5.4, ambapo dola bilioni 1.3 zilitakiwa kutoka Marekani na dola bilioni 1.2 kutoka China.
Lakini tangu kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House, Washington imetangaza kupunguza kwa kiasi kikubwa misaada yake ya kigeni, na Umoja wa Mataifa umekuwa ukisubiri maamuzi kuhusu operesheni za kulinda amani.
Marekani sasa imeuarifu Umoja wa Mataifa kwamba itachangia tu dola milioni 682 kwa bajeti ya 2025-2026, ikiwa ni pamoja na dola milioni 85 zilizotengwa kwa ajili ya ofisi ya baadaye ya Umoja wa Mataifa kwa ujumbe mpya wa kimataifa wa kupambana na magenge nchini Haiti.
Kwa jumla, Umoja wa Mataifa unatarajia upungufu wa 16% hadi 17% ya bajeti ya sasa ya kulinda amani.
Kusubiri uamuzi wa Marekani, misheni kumi na moja zinazofanya kazi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa zilikuwa zimetayarisha mipango ya kutarajia matukio mbalimbali ya kupunguza ufadhili.
Kupunguzwa kwa 25% kwa wanajeshi kutasambazwa kati ya misheni 11, afisa huyo amebainisha.
“Tunajua kutakuwa na matokeo katika suala la ufuatiliaji wa usitishaji mapigano, ulinzi wa raia, na kufanya kazi na wasaidizi wa kibinadamu,” amebainisha, akitabiri athari “muhimu” bila kuwa na uwezo wa kutathmini kwa undani zaidi.
Umoja wa Mataifa una walinda amani waliotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kusini mwa Lebanon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Sahara Magharibi.