
Viongozi mbalimbali duniani wamekaribisha tangazo la kusitishwa vita Ghaza kufuatia siku tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas na utawala wa kizayuni Israel nchini Misri kulingana na mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Trump alisema mapema leo Alkhamisi kuwa Israel na Hamas zimetia saini awamu ya kwanza ya mpango wake wa Ghaza, ambao unahusisha pamoja na mambo mengine kubadilishana mateka na wafungwa, kuingizwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza, na kuondoka hatua kwaa hatua jeshi la Israel katika eneo hilo la ardhi ya Palestina.
Inatarajiwa kuwa, ndani ya saa 72 baada ya kusainiwa makubaliano hayo, mateka 20 wa Israel na miili ya wengine 28 itaachiliwa makabala wa kubadilishana wafungwa wapatao 2,000 wa Kipalestina, kulingana na orodha iliyotolewa na Hamas.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameuelezea mpango huo kama “fursa muhimu”, akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaunga mkono “utekelezaji kamili” wa makubaliano hayo, kuongeza utoaji wake wa misaada ya kibinadamu, na kuendeleza juhudi zake za ujenzi mpya huko Ghaza.
Guterres ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika vita kufuata masharti ya mkataba huo, akisisitiza, kuwa “mateso (ya Wapalestina) lazima yahitimishwe.”
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesisitiza kuwa, “Malaysia inasimama kwa mshikamano kamili na watu wa Palestina katika harakati zao za kutafuta haki, utu na utaifa”.
Umoja wa Ulaya umeeleza katika taarifa iliyotolewa na Rais wa Kamisheni yake Ursula von der Leyen kwamba utaendelea kupeleka misaada huko Ghaza wakati huu na kusaidia katika ujenzi mpya wa eneo hilo la Palestina hapo baadaye.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yeye ameonyesha kuridhishwa na makubaliano hayo sambamba na kutuma salamu zake kwa Wapalestina na Muqawama wao ambao amesema, “licha ya majanga na masaibu yote waliyopitia, hawajayumba kwenye misimamo yao ya kuheshimika”.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema anakaribisha mpango wa kusitisha mapigano Ghaza, na kuhimiza kwamba lazima utekelezwe kikamilifu bila kuchelewa.
Viongozi wengine waliotoa taarifa na kauli za kukaribisha makubaliano ya kusitisha vita Ghaza ni pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa New Zealand Winston Peters, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na wizara za mambo ya nje za China na Japan…/