Bunge la Uhispania limeidhinisha vikwazo vya silaha vilivyopendekezwa na Waziri Mkuu Pedro Sanchez dhidi ya utawala wa kizayunii wa Israel.

Bunge hilo limeunga mkono agizo lililotangazwa mwezi Septemba na Sanchez kwa kura 178 zilizounga mkono dhidi ya 169 zilizopinga.

Waziri mkuu huyo wa Uhispania mwenye misimamo ya kisoshalisti alipiga marufuku kununua au kuiuzia silaha Israel muda mfupi baada ya utawala huo wa kizayuni kuishambulia kijeshi Ghaza kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya ngome za utawala huo ghasibu.

Jopo la wanahistoria, wataalamu wa sheria na wasomi wamevitaja vita vya Israel dhidi ya Ghaza kuwa ni mauaji ya kimbari.

Sanchez amekuwa mmoja wa wakosoaji wakali zaidi kati ya viongozi wa ulimwengu wa vita vya kinyama vya miaka miwili vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina.

Mnamo mwezi Septemba, Waziri Mkuu wa Uhispania alitangaza amri ya utekelezaji ya “kuipa sura kamili ya kisheria” marufuku aliyoweka, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa hatua dhidi ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.

Marufuku iliyoidhinishwa rasmi na bunge inapiga marufuku usafirishaji wote wa vifaa vya ulinzi, bidhaa au teknolojia kwa Israel na uagizaji wa bidhaa kama hizo kutoka kwa utawala huo wa kizayuni.

Sanchez ameikuwa akiikosoa jamii ya kimataifa kwa kushindwa kusitisha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, akishutumu mataifa makubwa kwa “kutojali” na “kushirikiana” na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyah katika jinai zake.

Uhispania ilikuwa moja ya nchi za kwanza za Ulaya kulitambua taifa la Palestina mwaka jana. Nchi nyingine kadhaa kubwa za Magharibi, zikiwemo Canada, Uingereza na Ufaransa, zilichukua hatua hiyo mwezi uliopita…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *