Bagamoyo. Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema yeye ni mzima wa afya: “Sina hata kichomi, wanaoniombea mabaya watatangulia wao mimi nitakuja kushiriki mazishi.”

Kikwete ambaye alikuwa Rais wa Tanzania (2005-2015) amesema hayo leo Ijumaa, Oktoba 10, 2025 katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Mkutano huo umefanyikia Uwanja wa Uwanja wa Mwakalenge, Bagamoyo ukihusisha majimbo ya Bagamoyo na Chalinze, Mkoa wa Pwani.

Kikwete amezungumzia afya yake baada ya baadhi ya mitandao ya kijamii kutoa taarifa potofu kwamba Rais huyo mstaafu amefariki dunia.

Kabla ya Kikwete ambaye ni mkazi wa Msoga, Jimbo la Chalinze kufikia kuelezea afya yake, alikuwa akizungumzia mafanikio ya CCM na uimara wa kuendelea kuongoza kwa muda mrefu.

Amesema Bagamoyo imeendelea kuwa ngome ya chama hicho na hilo linatokana na utekeleza wa kile inachokiahidi ikiwemo kuwa na Ilani nzuri inayoelezea kipi itakifanya ngazi ya mikoa na jimbo.

“Ujumbe kwako, bado safari hatujafika pale tunapotaka kufika, ipo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu, ninachofurahi CCM ikiahidi inatimiza.

New Content Item (1)

Mambo mazuri yanafanyika na tunataka mazuri zaidi,” amesema Kikwete.

Mwenyekiti huyo mstaafu huku akishangiliwa amesema: “Ilani imedadavua kila mkoa mambo gani yatafanyika na kila jimbo. Ndio maana nasema chama chetu kinaendelea kuchaguliwa, ukisema mzee huyu kwa nini asipumzike, wengine wanasema nimekufa, mimi mzima, sina hata kichomi, wanaoniombea mabaya watatangulia wao mimi nitakuja kushiriki mazishi.”

Kikwete amempongeza Dk Nchimbi kwa nafasi hiyo aliyoipata: “Unafanya kazi nzuri ya kukisemea Chama cha Mapinduzi, kwanza nimefurahi kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Samia Suluhu Hassan.”

“Ni chaguo sahihi kwa uongozi wa nchi yetu na wakati tulionanao sasa.

Nakufahamu tangu ukiwa kijana hadi umri uliofikia sasa,” amesema Kikwete.

Alichokisema Nchimbi

Dk Nchimbi amempongeza Kikwete akisema anazidi kutuonesha kwa vitendo kwamba kazi ya chama haina kikomo.

Dk Nchimbi amesema CCM miaka mitano ijayo inakwenda kuboresha fukwe za Bagamoyo, kukamilisha stendi ya Bagamoyo, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, madarasa, nyumba za walimu na watumishi wa afya.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ahadi zingine ni ujenzi wa duka kubwa: “Tukipiga Shopping Mall moja hapa si tunakwenda kumpa heshima Kikwete.” Pia, ujenzi wa barabara mbalimbali za Bagamoyo.

Dk Nchimbi amesema miradi ya maji inakwenda kupanuliwa ili kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma karibu na makazi yao.

“Ninachowaomba, jitokezeni Oktoba 29 kumchagua Samia awe Rais wetu, wabunge na madiwani,” amesema.

Yaliyofanyika Bagamoyo

Mgombea ubunge wa Bagamoyo, Subra Mugalu amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika kipindi cha miaka minne iliyopita wamepokea Sh27 bilioni za miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema fedha hizo zimetumika kwenye sekta za afya kwa kujenga majengo na vifaa tiba ambavyo vimesaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito: “Na kwa mwaka huu hakuna kifo hata kimoja cha mama mjamzito na huyu ndiyo Samia.”

Mugalu aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati amesema Halmashauri ya Bagamoyo yenye majimbo ya Bagamoyo na Chalinze imetekeleza miradi ya elimu ikiwemo shule ya Amali.

New Content Item (1)

Amesema miradi ya maji imetekelezwa ukiwamo mradi mkubwa unaoanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kwa zaidi ya Sh70 bilioni na upatikanaji wa maji umefikia asilimia 95.

Amesema Agosti 2025, Rais Samia aliipandisha hadhi hadi Halmashauri yao ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji ambayo imekuja na mabilioni ya fedha za kutekeleza Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (Tactic).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *