Kocha wa Bafana Bafana, Hugo Broos, ameahidi kikosi chake kitapambana kama simba kitakapokutana na Zimbabwe katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, leo Ijumaa Oktoba 10, 2025.
Hii ni mechi ya tisa kati ya kumi katika kampeni ya kufuzu kwa Bafana Bafana, ambapo kocha huyo raia wa Ubelgiji amesema anaamini kila mchezaji aliyemuita kikosini yupo tayari kupambana kwenye mechi hiyo itakayopigwa mjini Durban.
Broos amesema malengo yao ni kuhakikisha wanaifunga Zimbabwe ili kufanikisha safari ya kufuzu kwenye fainali hizo, ambazo kwa mara ya kwanza zitashirikisha mataifa 48, katika nchi za Marekani, Mexico na Canada.
“Hakuna kilichobadilika. Ninaamini bado kundi ni gumu, lakini Bafana Bafana tunaamini tuna kila sababu ya kuendelea kupambana ili kushinda mchezo wa leo, na mchezo wa mwisho ambao tutacheza dhidi ya Rwanda.
“Kikosi changu ni kile kile, ubora bado ule ule, hivyo sina shaka na mipango tuliyojiwekea katika uwanja wa mazoezi ili kufanikisha lengo letu,” amesema.
“Mechi itaanza saa 12 jioni kwa saa za hapa (Afrika Kusini), nitawahimiza wachezaji wangu kupambana kama simba kwa sababu tunataka kushinda mechi hii.
“Lazima tupambane kwa bidii ili kumfurahisha kila mtu wa taifa hili na shabiki yetu yoyote ambaye yupo nje ya Afrika Kusini.”
Naye kipa na nahodha wa Bafana Bafana, Ronwen Williams, amesema wamejiandaa vizuri na wanatarajia kufanya kazi kwa bidii kwenye uwanja wa mechi ili kuhakikisha wanapata pointi muhimu dhidi ya Zimbabwe (leo Ijumaa) na Rwanda (Jumanne ijayo).
“Tunajua madhara ya kukosa matokeo katika michezo hii miwili, ndio maana sisi wachezaji na kocha wetu tumejiandaa kuzipigania pointi zote sita ambazo zitakuwa njia nzuri ya kutufikisha tunapotaka kufika. Hii ni sehemu muhimu ya kwetu, hatutaki kwenda tofauti na malengo tuliojiwekea, tumehimizana kucheza kwa umoja na ushindikiano kwango kikosi chetu bado kipo vilevile kwa miaka miwili au mitatu iliyopita.” amesema Ronwen Williams
HALI YA KUNDI C
Kwa sasa, Afrika Kusini inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi C, ikiwa nyuma ya Benin kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, Benin inakabiliwa na ratiba ngumu zaidi, ikiwa na mechi za ugenini dhidi ya Rwanda na Nigeria.
Fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2026 zitafanyika Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026 zikihusisha mataifa 48, zikiwa ndio fainali kubwa zaidi, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930.