
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unapanga kupunguza kwa asilimia 25 vikosi vyake vya kulinda amani
Taarifa zaidi zinasema kuwa, Umoja wa Mataifa utalazimika kupunguza vikosi vyake vya kulinda amani duniani kote kwa takribani asilimia 25 kutokana na kukosekana fedha.
Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema vikosi hivyo vitapunguzwa kutokana na ukosefu wa fedha, unaohusishwa zaidi na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani.
Takribani wanajeshi na askari polisi 13,000 hadi 14,000, pamoja na vifaa vyao watarudishwa makwao, huku idadi kubwa ya wafanyakazi wa kiraia wa vikosi hivyo pia ikiathiriwa.
Marekani ilikuwa inatarajiwa kuchangia dola bilioni 1.3 kati ya jumla ya bajeti ya dola bilioni 5.4 kwa shughuli za kulinda amani za 2025 hadi 2026 katika maeneo mbalimbali duniani.
Hata hivyo, serikali ya Marekani imeueleza Umoja wa Mataifa kwamba, italipa tu nusu ya kiasi hicho, au dola milioni 682 ambazo zinajumuisha dola milioni 85 zilizotengwa kwa ajili ya kikosi kipya cha kimataifa cha kupambana na magenge ya uhalifu nchini Haiti, ambacho hakikuwepo katika bajeti ya awali.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wataalamu wa mambo wamekuwa wakikosoa utendaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa katika baaadhi ya mataifa vinakohudumu kutokana naa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.