Dar es Salaam. Wakati mabalozi wa nchi za Scandinavia wakieleza mikakati ya kuendelea kushirikiana na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) katika miradi ya maendeleo, shirika hilo limeahidi kutumia fursa hiyo kujikita zaidi katika miradi ya maendeleo kupitia ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).

Mabalozi wa nchi za Sweden, Norway, Denmark na Finland nchini Tanzania leo, Oktoba 10, 2025, wametembelea na kukagua miradi ya afya na elimu inayotekelezwa na shirika hilo kwa ushirikiano na nchi hizo.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaad (wa kwanza kushoto), akifuatiwa na Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Ozaki Macias, katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shillingi (katikati), kushoto ni
Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting na balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes

Katika ziara hiyo iliyoanzia makao mkuu ya Shirika la Elimu Kibaha, mabalozi hao walitembelea Shule ya Msingi Tumbi, Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha na Shule ya Sekondari Tumbi na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya ukaguzi na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi, mabalozi wa nchi hizo wamesema ushirikiano wa Nordic na Shirika hilo umekuwa na tija na kuahidi kuuendeleza katika nyanja za elimu na afya.

Awali katika ziara hiyo, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji, mabalozi hao walihoji mafanikio na changamoto kwenye mradi, ufaulu katika shule ambazo ziko kwenye mradi, uwiano wa walimu na wanafunzi na hali ya malipo ya ada katika elimu.

Wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi, baadhi ya watumishi wa shirika hilo wamesema mafanikio yanachangiwa na huduma bora inayotolewa.

Katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, uongozi wa shule ulisema uwiano kati ya wanafunzi na walimu ni mwalimu mmoja kwa watoto 50 na kubainisha uwezo wa wanafunzi na ufaulu ambao walisema unachagizwa na mambo mengi, ikiwamo motisha, bajeti ya vifaa vya kufundishia na walimu na mambo mengine mengi.

Mabalozi wa nchi hizo wamesema mradi umekuwa chachu ya maendeleo tangu ulipoanzishwa mwaka 1963 na kuendelezwa na viongozi wa awamu zote waliofuatia, hivyo kama nchi za Scandnavia wataendeleza ushirikiano huo kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaad amesema mpango wa mradi huo ni kwa vizazi vijavyo, akigusia upande wa elimu na kueleza kuwa inafanyika kwa kiwango cha juu, vivyo hivyo kwenye afya.

Balozi wa Finland, Theresa Zitting amesema mradi umekuwa ukiimarika kila mwaka na kuutaja kuwa wa mfano nchini.

Balozi wa Sweden, Charlotta Ozaki Macias amesema wataendelea kuunga mkono mradi huo huku akigusia namna ushirikiano uliopo kati yao na Shirika umekuwa na tija kitaaluma kwenye  shule na vyuo vikuu.

Wakati balozi wa Norway, Tone Tinnes ameeleza kwamba ubora wa miradi inayofanywa kwa ushirikiano wao na Shirika ni mwelekeo mzuri kwa vizazi vijavyo na wao wataendeleza ushirikiano huo katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Akizungumzia ushirikiano huo na mkakati wa kupanua wigo katika miradi mbalimbali ya maendeleo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha,  Robert Shillingi amesema wataendelea kutumia ardhi kubwa waliyonayo ili kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo.

“Tunazidi kuangalia fursa kwa kuwatumia wadau wengine wa maendeleo  kuingia katika miradi miradi ya ubia wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP)

“Serikali inachagiza katika masuala ya namna hii kushirikiana na sekta binafsi kutoa huduma stahiki na zenye matokeo ili kuiletea maendeleo ya nchi, hivyo tutaitumia fursa iliyopo ya ushirikiano na wenzetu kufanikisha hili,” amesema.

Mradi ya Elimu na huduma za Afya Kibaha  ilianzishwa mwaka 1963 ukifanyika kwa ushirikiano wa nchi za Scandnavia na Shirika la Elimu Kibaha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *