Mwanza. Wadau wa Bonde la Ziwa Victoria wametakiwa kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa Sh245 bilioni zinazohitajika kutekeleza mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji wa bonde hilo kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka 2025 hadi 2045.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 9, 2025 katika jukwaa la wadau wa sekta mtambuka katika usimamizi wa rasilimali za maji lililofanyika jijini Mwanza, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday amesema utekelezaji wa mpango huo unahitaji Sh245 bilioni, sawa na wastani wa Sh12.25 bilioni kwa mwaka.

Amewataka kushirikiana kuhakikisha fedha hizo zinapatikana kupitia vyanzo vya ndani ikiwemo ada za matumizi ya maji.

Mkurugenzi wa LVBWB, Dk Renatus Shinhu kiwsilisha mada wakati wa jukwaa la wadau wa sekta mtambuka katika usimamizi wa rsilimali za maji lililofanyika jijini Mwanza.

“Katika muktadha huo, mkutano wa leo una kazi ya kujadili upatikanaji wa fedha hizo,” amesema Sunday.

Amesema tathmini ya Umoja wa Afrika ikishirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika na Shirika la Global Worker Partnership imeonyesha kuwa ili bara la Afrika lifikie malengo endelevu ya kimataifa ifikapo mwaka 2030, zinahitajika dola za Marekani milioni 30 kwa mwaka kwa ajili ya sekta ya maji, ambapo asilimia 60 ya fedha hizo zinaweza kupatikana kupitia vyanzo vya ndani.

Sunday amesema usimamizi wa rasilimali za maji nchini unaongozwa na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 (toleo la mwaka 2005) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji namba 11 ya mwaka 2009 na marekebisho yake namba 8 ya mwaka 2022.

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa majukwaa ya wadau ni hatua muhimu inayowawezesha washiriki kujadiliana changamoto na fursa katika usimamizi wa maji, kupanga mikakati ya pamoja na kufanya maamuzi jumuishi yanayozingatia maslahi ya wote.

Amesema jukwaa hilo lina jukumu la kutengeneza mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji wa bonde hilo, kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wake, pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini.

Akizungumzia changamoto, Sunday amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri mzunguko wa mvua na kuongeza upungufu wa maji katika maeneo mengi ya bonde la Ziwa Victoria, hali inayohitaji mikakati madhubuti ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameongeza kuwa jukwaa la wadau linapaswa kukutana angalau mara mbili kwa mwaka na majukwaa ya madakio yafanyike kila robo mwaka ili changamoto zinazojitokeza katika ngazi ya chini ziweze kuwasilishwa na kutafutiwa suluhisho katika jukwaa kuu.

Amesema jukwaa hilo la sita pia lina lengo la kuwasilisha mapendekezo ya mapitio na mabadiliko ya ada za matumizi ya maji pamoja na kuwasilisha mpango wa pamoja wa usimamizi wa rasilimali hizo kwa bonde la Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Bonde hilo, Emmanuel Ntemi amesema lengo kuu la jukwaa hilo ni kuimarisha ushirikiano na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji.

Amesema maji ni rasilimali mtambuka inayohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuepuka migongano na changamoto za usimamizi.

Mkurugenzi wa LVBWB, Dk Renatus Shinhu kiwsilisha mada wakati wa jukwaa la wadau wa sekta mtambuka katika usimamizi wa rsilimali za maji lililofanyika jijini Mwanza.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Dk Renatus Shinhu amesema licha ya changamoto za uharibifu wa mazingira, bonde hilo limefanikiwa kujenga zaidi ya vituo 23 vya hali ya hewa na vituo 21 vya kusoma mwenendo wa maji kwenye mito, mabwawa na ziwa.

Pia imefanikiwa kuchimba mabwawa saba na visima, pamoja na kuhifadhi vyanzo 25 vya maji kwa kuweka vigingi na mabango ya onyo la wanaojihusisha na ufanyaji shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji.

Amesema pia wameunda jumuiya 32 za watumiaji wa maji na kuanzisha ofisi ndogo katika ngazi za vidakio ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Jukwaa hilo lililodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limehusisha washiriki kutoka wizara na taasisi za serikali zinazohusika na maji, mazingira, uvuvi na rasilimali asili, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za elimu ya juu na utafiti, sekta binafsi pamoja na jumuiya za watumiaji wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *