Mbeya. Ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini, wanafunzi wa shule za sekondari wameishauri Serikali kuanzisha masomo ya kujitegemea na ujasiriamali ili kumuandaa mhitimu kujitegemea.
Wakizungumza wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wilaya ya Mbeya mkoani hapa, baadhi ya wanafunzi wamesema Elimu ya Kujitegemea (EK) na somo la Ujasiriamali vinaweza kuwa mkombozi kwa vijana kutegemea ajira za Serikali.
Paulina Mtujilwa, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Maghabe amesema ili kuondokana na foleni ya vijana kusubiri ajira za Serikali, wizara inaweza kuanzisha masomo ya kujitegemea ikiwamo ujasiliamali.
Amesema masomo ya kujitegemea yanaweza kuanzia elimu ya msingi ili kumuandaa mwanafunzi anapomaliza elimu yake kuendesha maisha na muda mwingine kujiajiri.
“Kupitia elimu ya kujitegemea, mwanafunzi anaweza kujiajiri na kuendesha maisha yake na muda mwingine kuajiri wenzake, mathalani katika kilimo na ufugaji,” amesema Paulina.
Kwa upande wake, Shozi Samuel amesema kama ambavyo Serikali ilifanikiwa kuandaa shule za vipaji maalumu, hivyo inaweza kuweka misingi ya elimu ya ujasiliamali kuanzia ngazi ya chini na kuondokana na kilio cha ajira kwa wahitimu.
Amesema pamoja na baadhi ya shule kuwa na masomo ya ziada ikiwamo sekondari Maghabe, lakini ikiwekea msukumo kwa shule zote nchini inaweza kuokoa kundi kubwa la wahitimu kubaki mtaani.
“Sisi wa masomo ya Sayansi ndio muhimu zaidi kuwa na elimu ya ujasiliamali hasa upande wa kilimo kutambua mbegu bora, hii inaweza kusaidia kundi la wahitimu kutegemea ajira za Serikali,” amesema Samuel.
Mkuu wa shule hiyo, Albina Robert amesema katika kutambua maisha ya mtoto pamoja masomo rasmi ya darasani, lakini ipo elimu ya ujasiliamali kumuandaa mwanafunzi kujitegemea.
Amesema kwa kuwa shule hiyo ipo katika mazingira ya kilimo cha umwagiliaji, yapo masomo ya ziada yanayogusa maeneo hayo akieleza kuwa matarajio ni kumuweka mtoto katika soko la ushindani.
“Tuna elimu ya mifugo, kilimo cha umwagiliaji na ujasiliamali ambapo tunamuandaa mtoto kujiweka kwenye soko la ajira, lakini hatujasahau maadili na dini kumuweka mwanafunzi kumjua Mungu,” amesema Albina.
Mkuu huyo ameongeza kuwa kutokana na misingi hiyo, shule hiyo imekuwa na matokeo mazuri akitolea mfano mwaka jana kupata ufaulu wa daraja la kwanza, la pili na tatu, akifafanua kuwa kwa sasa uongozi unajitahidi kufuta daraja la tatu.
Kuhusu mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, mkuu huyo wa shule amesema zinahamasisha uzalendo na kuteleleza falsafa ya kupambana na rushwa, malaria, afya na mazingira mazuri ya lishe.
“Kwa kuwa ipo mipango ya kuwapo kwa viwanda katika halmashauri yetu, tunatarajia wanafunzi wetu wawe sehemu ya wanufaika wa fursa hizi kwa kwa sababu maarifa wanayo na tumekuwa sehemu ya kujizalishia miti ya matunda na mbogamboga,” amesema mkuu huyo.
Akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia mbio za Mwenge wa Uhuru, kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Ismail Ally Ussi amewapongeza maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kubuni klabu za wanafunzi kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Amesema walimu wana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa klabu hizo na kutokuwa sehemu ya kukwamisha juhudi hizo kwa lengo la kuwa na Taifa bora na lenye maadili kupinga aina yoyote ya rushwa.
“Toeni elimu juu ya kupambana na vitendo vya rushwa, katika hili niwapoengeze maofisa wa Takukuru kwa kuweka klabu hizi za wanafunzi ambapo tunatarajia Taifa lenye misingi, weledi katika kupinga vitendo vyovyote vya rushwa,” amesema Ussi.