
Dar es Salaam. Wasichana wa kitanzania wameaswa kuzitumia vyema fursa za kiuchumi zinazojitokeza kutoka kwa Serikali na wadau wa maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na kuepuka vishawishi.
Hayo yamesemwa na Ofisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara ya Maendeleo ya Watoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Imelda Kamugisha alipokuwa akizungumza na baadhi ya wasichana wanufaika wa Mradi wa Ahadi unaofadhiliwa na Global Affairs Canada (GAC) na kutekelezwa na World Vision Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za Baba Watoto Centre na KIWOHEDE ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Dunuani.
Imelda amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau kuhakikisha wanatengeneza fursa na kuwajengea uwezo wasichana ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kufikia ndoto zao.
Aidha amewapongeza wadau hao kwa kutekeleza mradi wa Ahadi ambao unaowawezesha mabinti kwa kuwapatia mafunzo ya ujuzi mbalimbali ikiwemo ujasiriamali
“Mafunzo haya yanalenga kuwawezesha mabinti kujitegemea kiuchumi”amesema.
Kwa upandee wake Ofisa Mradi wa Ahadi, Martha Mdaki amesema kupitia mradi huo unaotekelezwa kwenye halmashauri za Ubungo na Ilala kwa mkoa wa Dar es Salaam vijana hususani wasichana walioko nje ya mfumo wa shule mpaka sasa umewafikia vijana 2,767 huku zaidi ya asilimia 70 ikiwa ni wasichana.
“Kupitia mradi huu vijana hususani wasichana wamepata fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi huku wengine wakipatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali ikiwemo ushonaji, utengenezaji wa sabuni na masuala ya urembo,” amesema Martha.
Ameongeza kuwa mbali na uwezeshaji wa shughuli za kiuchumi, vijana hao wamepatiwa elimu muhimu kuhusu afya ya uzazi na akili ili kuwaandaa kuwa viongozi bora wa kesho