Watoto wengine 21 wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambuio hilo la kikatili.

Kwa mujibu wa UNICEF kituo hicho kilikuwa kikihifadhi familia ambazo tayari zilikuwa zimeyakimbia makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan.

“Shambulio hili la kusikitisha dhidi ya watoto na familia ambazo tayari zimekimbia na kusaka usalama ni jambo la kushtua,” amesema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.

Ameongeza kuwa “Kuwaua na kuwajeruhi watoto ni ukiukaji mkubwa wa haki zao, na mashambulio dhidi ya raia katika maeneo yanayokusudiwa kutoa hifadhi ni jambo lisilokubalika kabisa.”

Wakimbizi wengi wakiwa wanawake na watoto waliokimbia machafuko El-Fasher

© UNICEF/Brice Kevin Da

Wakimbizi wengi wakiwa wanawake na watoto waliokimbia machafuko El-Fasher

El-Fasher chini ya mzingiro wa RSF

Mji wa El Fasher, makao makuu ya Kaskazini mwa Darfur, umekuwa chini ya mzingiro wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF kwa zaidi ya siku 500, hali iliyosababisha raia kukosa chakula, maji na huduma za matibabu.

Hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara na ukosefu wa mahitaji muhimu.

Kwa mujibu wa UNICEF, maeneo kadhaa ya Kaskazini mwa Darfur yamekuwa yakikabiliwa na baa la njaa kwa miezi kadhaa, na hali ya lishe duni kwa watoto imefikia kiwango cha janga.

Familia nyingi zinajikimu kwa posho ndogo mno, huku vituo vya afya vikiripoti vifo vingi vya watoto vinavyotokana na njaa na magonjwa yanayoweza kuzuilika. Uharibifu wa njia za usambazaji, uporaji wa misafara ya misaada, na vizuizi vya ufikiaji wa kibinadamu vimeifanya kazi ya kutoa misaada kuwa ngumu na karibu kutowezekana.

Familia iliyokimbia makazi yao huko Tawila baada ya kukimbia mapigano huko Al Fasher, Darfur Kaskazini.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Familia iliyokimbia makazi yao huko Tawila baada ya kukimbia mapigano huko Al Fasher, Darfur Kaskazini.

UNICEF imerejelea wito wake wa haraka kwa:

  • Kusitishwa mara moja kwa mapigano kote nchini Sudan na kuondolewa kwa mzingiro wa El Fasher.
  • Kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwemo kulinda raia na miundombinu ya kiraia.
  • Kupitishwa kwa usalama kwa watoto na familia zinazokimbia vurugu.
  • Upatikanaji salama na usiokatizwa wa misaada ya kibinadamu kwa jamii zilizoathirika.
  • Kuwawajibisha waliohusika na mashambulio dhidi ya raia, hususan watoto.

Licha ya changamoto za usalama na ufikiaji wa waathirika, UNICEF na washirika wake wanaendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha, ikiwemo huduma za afya, lishe, maji safi na usafi wa mazingira kwa watoto kote Sudan.

“Watoto nchini Sudan wamepitia mateso yasiyoelezeka,” ameongeza Russell. “Wanastahili amani, ulinzi, na fursa ya kuishi na kustawi.”

Familia zilizofurushwa makwao Tawola Jimbo la Darfur Kaskazini

ERR-Taweela

Familia zilizofurushwa makwao Tawola Jimbo la Darfur Kaskazini

Rais 57 wauawa ndani ya siku mbili: OCHA

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Raia OCHA limeyalaani vikali mashambulio yaliyolenga raia kaskazini mwa Darfur, kufuatia mlolongo wa mashambulio yaliyopelekea vifo vingi katika jimbo hhilo.

“Nayalaani kwa kauli kali zaidi mashambulio ya mara kwa mara na ya kulenga dhidi ya raia Kaskazini mwa Darfur,” amesema Denise Brown, Kaimu Mratibu Mkazi na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan.

Kati ya jioni ya 10 Oktoba na asubuhi ya 11 Oktoba, mashambulio ya ndege zisizo na rubani yani droni yaliyoripotiwa kufanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF, yaliangukia eneo lililokuwa kimbilio la watu waliofurushwa kwenye makazi yao katika mtaa wa Daraja Oula. Mashambulio hayo yalipelekea vifo vya raia 57, wakiwemo wanawake na watoto.

Hospitali ya Al Fasher huko Darfur imeangamia kwa kiasi kufuatia mashambulizi ya makombora mwezi Oktoba.

© Al-Saudi Maternity Hospital

Hospitali ya Al Fasher huko Darfur imeangamia kwa kiasi kufuatia mashambulizi ya makombora mwezi Oktoba.

Mashambulizi dhidi ya hospitali

Hadi hapo awali kati ya 5 na 8 Oktoba, mlolongo wa mashambulio, ikiwemo shambulio dhidi ya Hospitali ya Saudi kituo cha mwisho kikubwa cha afya kilichosalia kikifanya kazi El Fasher kiliarifu vifo vya takriban raia 53 na kujeruhi zaidi ya 60.

Hospitali hiyo, ambayo inahudumia maelfu ya raia walioathirika na mgogoro, iliathirika vibaya.

“Hospitali, kimbilio na sehemu za hifadhi hazipaswi kulengwa,” Brown amesema. “Tukio hili linahitaji uchunguzi wa kina na usioegemea upande wowote, na wale waliohusika lazima wachukuliwe hatua.”

Brown alirudia wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, kusitishwa mara moja kwa mashambulio dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, pamoja na upatikanaji salama wa misaada ya kibinadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa na washirika wake linaendelea kujitolea kusaidia watu wa El Fasher na wote walioathirika na mgogoro kote Sudan. Brown alisisitiza kwamba raia lazima walindwe, upatikanaji wa kibinadamu uhakikishwe, na vurugu kuishia mara moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *