Mgogoro huo, ambao Mkuu wa Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix ameuuelezea kama “mgumu kuliko wakati wowote ule,” unatokana na kutolipwa kwa sehemu ya michango iliyopangwa, ambayo ni ada za lazima zinazolipwa na nchi wanachama kufadhili shughuli za Umoja wa Mataifa katika maeneo hatarishi duniani kiwango kikiwa chini ya bajeti iliyopitishwa kwa mwaka 2025–2026.

Akihutubia maafisa wa ulinzi na wanadiplomasia katika mkutano wa ulinzi wa amani mjini New Delhi wiki hii, Lacroix alisema “Kwa bahati mbaya, hatuna njia nyingine.”

Akaongeza kuwa “Walinda amani wetu, walinda amani wenu, wanalinda watu  hao katika tofauti kati ya maisha na kifo kwa mamia ya maelfu ya raia.”

Afisa wa Polisi wa UN (UNPOL) akizungumza na wananchi wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

© MONUSCO/Kevin Jordan

Afisa wa Polisi wa UN (UNPOL) akizungumza na wananchi wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Kupunguzwa kwa kiwango kikubwa shughuli mashinani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameagiza operesheni zote za ulinzi wa amani kubaini maeneo ya kupunguza matumizi kwa asilimia 15 ya bajeti zao za kila mwaka, hatua ambayo itasababisha kupunguzwa kwa takribani asilimia 25 ya wafanyakazi wa kijeshi na kiraia kutokana na muda mfupi uliotolewa kutekeleza hatua hizo.

Mabadiliko hayo yataathiri kila eneo kuu la kazi za ulinzi wa amani kuanzia doria na jukumu la ulinzi, hadi usafirishaji, shughuli za anga na huduma za kiraia.

Idara ya Umoja wa Mataifa ya Operesheni za Amani (DPO) imeonya kuwa kupungua kwa walinda amani mashinani kutamaanisha doria chache za kufuatilia makubaliano ya kusitisha mapigano, maeneo machache salama kwa raia, na msaada mdogo wa kibinadamu katika maeneo kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Lebanon na Uwanda wa Golan.

Wito wa mshikamano

Bwana Lacroix amezihimiza “nchi zote wanachama kulipa michango yao kwa ukamilifu na kwa wakati” na ametoa wito wa ushirikiano wa pamoja kupinga kile alichokiita kampeni za upotoshaji kuhusu shughuli za ulinzi wa amani.”

Amesema “Tunahitaji uelewa na msaada wenu, lakini pia tunapaswa kufanya kazi pamoja kurekebisha hali hii”.

Katibu Mkuu António Guterres, akizungumza wiki iliyopita na nchi zinazochangia vikosi na polisi kwa shughuli za ulinzi wa amani, alisisitiza umuhimu wa operesheni hizo.

Hata hivyo, alisema, bila ufadhili wa uhakika, wa kutosha na wa wakati, shughuli za ulinzi wa amani haziwezi kutekeleza majukumu yaliyowekwa na Baraza la Usalama.

Wanajeshi wa kulinda amani wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) wameongeza uwepo wao na kuimarisha doria za magari, wakipitia njia za udanganyifu, zilizojaa mvua mchana na usiku.

UNMISS/Denis Louro

Wanajeshi wa kulinda amani wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) wameongeza uwepo wao na kuimarisha doria za magari, wakipitia njia za udanganyifu, zilizojaa mvua mchana na usiku.

Bajeti katika shinikizo kubwa

Mwezi Julai, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliidhinisha bajeti ya dola bilioni 5.38 kwa shughuli za ulinzi wa amani kwa mwaka 2025–2026, ikishuka kidogo kutoka dola bilioni 5.6 za mwaka uliopita.

Bajeti hiyo inagharamia operesheni pamoja na vituo vya kimataifa vya usaidizi vilivyoko Entebbe Uganda na Brindisi Italia.

Hata hivyo, utekelezaji wa bajeti hiyo unategemea michango halisi inayopokelewa.

Shughuli za ulinzi wa amani zinachukua chini ya nusu ya asilimia moja ya matumizi ya kijeshi duniani, yaliyokadiriwa kufikia dola trilioni 2.7 mwaka 2024, lakini bado zinabaki kuwa miongoni mwa zana muhimu zaidi za Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Mkuu wa zamani wa Mpango Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Cyprus UNFICYP, Colin Stewart, kabla ya kustaafu alisema “Watu wengine hujiuliza kwa nini operesheni za ulinzi wa amani bado zinahitajika.
Jibu ni rahisi “kuna amani kwa sababu misheni hizo zimekuwa zikifanya kazi yake. Bila hiyo, kutoaminiana kati ya pande husika kungeweza kubadilika haraka kuwa mapigano.”

Hatua ya muhimu

Tangu mwaka 1948, zaidi ya walinda amani milioni mbili kutoka nchi wanachama wamefanya kazi katika mazingira hatarishi duniani kote, wakitekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano na kuweka fursa kwa mazungumzo ya kisiasa na mchakato wa amani.
Zaidi ya walinda amani 4,400 wamepoteza maisha wakitafuta amani ya kudumu.

Umoja wa Mataifa unapoadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa, Bwana Lacroix amesema shirika hilo liko katika “hatua muhimu ya mabadiliko, na lazima libadilishe shughuli zake za amani kulingana na uhalisia mpya wa dunia”.

Ameonya kuwa “Changamoto zilizopo mbele yetu ni za kweli lakini vivyo hivyo uwezo wetu wa kukabiliana nazo ikiwa tutabaki wamoja kwa lengo, wa vitendo katika utekelezaji, na thabiti katika dhamira yetu ya kudumisha amani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *