Kwa sasa nchini Tanzania, habari kuu zinazogonga vichwa vya habari ni mwenendo wa kampeni zinazozidi kuchanja mbuga. Lakini wananchi wengi wanaonyesha kutoridhishwa na namna waandishi wa habari wanavyoripoti kuhusu kampeni za uchaguzi Wengine wakisema ripoti nyingi ziko kama matangazo.
Na mamlaka nchini humo pia zimekuwa zikivinyooshea kidole baadhi ya vyombo vya habari kwa madai ya kukiuka maadili na sheria nyakati za uchaguzi.
Wiki chache zimebaki hili likoje kwa mwaka huu? Edwin Soko, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Tanzania (MISA) alisema “Ni kuanzia kampeni zilipoanza Agosti mwaka huu hatukuwa na mikasa ama madhila dhidi ya waandishi wa habari ambayo tumeyarekodi… Kwa hiyo unaweza kuona ni jinsi gani vyombo vya habari vimekuwa na weledi mkubwa..”
Waandishi wanahitaji utambulisho zaidi
Mbali na kutakiwa kutambulika na bodi ya ithibati ili kupata ruhusa ya kuandika habari za uchaguzi, mwaka huu waandishi wa habari, wanalazimika kupata tena kibali kutoka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ili waweze kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Kutupiliwa mbali kwa baadhi ya habari, maeneo ya pembezoni kutokupewa kipaumbele, wagombea wasio na ukwasi kutotengeneza habari, ni kilio cha muda mrefu nyakati za uchaguzi navyo pia ni changamoto katika uzalishaji wa habari.