Wananchi hawa wakizungumza na DW Swahili katika vijiji vya Majengo, Nanguruwe na Tangazo wilayani Mtwara, wamesema licha ya hamasa ya uchaguzi kuongezeka, wengi bado hawajapewa nafasi ya kusikia sera zinazogusa moja kwa moja maisha na changamoto wanazozipitia.

Wanadai kwamba kampeni nyingi, hasa za wagombea wa nafasi za urais, hufanyika mijini zaidi. Wanasema wanasikiliza tu habari kwenye vyombo vya habari. Cecilia Anthony “Kwa sisi huku kwetu tunatamani wagombea waje, waje kabisa watusikie sisi wananchi tunasema nini au tunahitaji nini kwao”.

Mwananchi mwingine Hussein Banda alisema “Mimi nachojuwa mgombea ananadi sera zake na baadaye lazima tupewe nafasi ya kuuliza maswali lakini nashangaa kwa mwaka huu, hata mgombea mmoja hakuna aliyetoa nafasi ya kuuliza maswali haijatokea kwa mwaka huu”.

Uchaguzi Tanzania | Wananchi wakimsikiliza mgombea wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo
Wananchi wakimsikiliza mgombea wa chama cha upinzani cha ACT-WazalendoPicha: Ericky Boniphase/DW

Makundi yalalamika kutengwa

Kundi la wanawake ambao hawafungamani na vyama vya siasa limesema mara nyingi sauti zao hazisikilizwi wakati wa kampeni za uchaguzi hivyo changamoto zao hazishughulikiwi.  Wengi wanakabiliana na changamoto za ukosefu wa maji safi na salama, miundombinu mibovu ya barabara na upatikanaji duni wa huduma bora za afya.

Wanawake hawa wanataka wanasiasa wafike kwenye maeneo yao ili wasikilize matatizo yao na kuonyesha mipango yao ya maendeleo kwa vitendo, siyo kutoa maneno tu.

Vijana nao wanataka kampeni zenye maudhui ya sera badala ya maneno ya malumbano yaliyojaa kashfa na chuki dhidi ya wagombea, hasa wale wanaowania nafasi za udiwani na ubunge. Matarajio yao ni kuona wagombea wakieleza mipango yao kwa uwazi na kuonyesha jinsi watakavyoshughulikia changamoto zinazowaathiri moja kwa moja.

Tanzania Arusha | Mgombea wa urais kupitia chama cha CCM - Samia Suluhu Hassan
Mgombea Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za urais jijini Arusha, TanzaniaPicha: CCM

Hadija Mpoto alisema “Hawa wagombea wanapofika, waje watupe dira ili tujuwe sisi tunaenda wapi endapo tukimchagua mgombea huyo”.

Mchambuzi: Hii inaashiria pengo kati ya wagombea na raia

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Bartazar Komba kutoka shirika lisilo la kiserikali la Faidika Wote Pamoja hapa mkoani Mtwara anasema mitazamo hiyo inaonyesha pengo kubwa la mawasiliano kati ya wagombea na wananchi wa vijijini. “Moja ya dhamira ya demokrasia ni kuleta watu wengi ili kuwe na machaguo mengi ya wananchi lakini kwa hali inayoendelea sasa inaonekana maana halisi ya demokrasia inafifishwa..”

Kwa mujibu wa rekodi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jumla ya vyama 17 vimesimamisha wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29. Hata hivyo, hadi sasa, ni wagombea wasiozidi watano pekee waliowasili mkoani Mtwara kunadi sera zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *