KISUMU – Maelfu ya waombolezaji kutoka jiji la Kisumu na maeneo mengine ya Magharibi mwa Kenya wamejitokeza siku ya Jumamosi kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kiongozi mashuhuri, aliyetawala siasa za eneo hilo katika kipindi chote cha uhai wake.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kisumu ndio iliyokuwa ngome kuu ya kisiasa ya Odinga, jiji ambalo aliishi akiwa mtoto mdogo. Maelfu ya waombolezaji, wadogo kwa wakubwa kuanzia Alfajiri walifurika nje na ndani ya uwanja wa michezo wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Mamboleo, kuutazama mwili wa kiongozi wao.

Uwanja wa Mamboleo Kisumu
Uwanja wa Mamboleo Kisumu © JASON SAGINI

“Kufariki dunia kwa Baba yetu Raila, kumetuacha mayatima” Benter Achieng mmoja wa waombolezaji aliiambia RFI Kiswahili. Edwin Ochieng, mwanasiasa chipukizi jijini Kisumu, amesema atamkumbuka Raila kwa ujasiri wake wa kupigania demokrasia na haki za watu wanyonge.

“Ametuacha na somo kubwa la kupambania haki za watu wa kawaida katika nchi hii” Amesema Ochieng.

Wakaazi wa Kondele Kisumu wakiomboleza kifo cha Raila Odinga
Wakaazi wa Kondele Kisumu wakiomboleza kifo cha Raila Odinga © JASON SAGINI

Majonzi, maumivu

Waombolezaji wamesikitishwa na uamuzi wa serikali kutousafirisha mwili wa kiongozi huyo kwa barabara, na badala yake kuusafirisha mwili wake kwa helikopta hadi uwanjani.

“Nimesitika kuwa hatukupata fursa ya kutembea na baba barabarani, tutembee naye, tukimwimbia” Beatrice Anyango, amesikitika.

Christine Auma, alilala uwanjani, kutoka Ijumaa iliyopita, lakini hakufanikiwa kuuaga mwili wa baba.

“Nimekesha hapa uwanjani. Sijala tangu baba alipofariki dunia. Sijui tutaishije bila Raila. Alikuwa mtetezi wetu” amesema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, atazikwa siku ya Jumapili nyumbani kwao Bondo, katika kaunti ya Siaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *