Akihutubia nchi wajumbe 195 wa UNCTAD mjini Geneva hii leo, Katibu Mkuu wa UNCTAD Rebeca Grynspan amesema kuwa asilimia 72 ya biashara ya dunia “bado inaendelea chini ya kanuni za Shirika la Kimataifa la Biashara Duniani WTO” hii ikimaanisha Shirika la Biashara Duniani, ambapo makubaliano yake yanaridhiwa na kusainiwa na nchi zinazoshiriki biashara.
“Tumepiga hatua kuepuka mnyororo wa kuongezeka kwa ushuru ambao mara moja ulipeleka uchumi wa dunia kwenye mdororo katika miaka ya 1930,” Bi. Grynspan amewaambia wajumbe wa UNCTAD waliokusanyika Geneva kuendeleza juhudi za kuondoa mamilioni ya watu kwenye umasikini kupitia biashara.
“Hii haikutokea kwa bahati mbaya, ilitokea kwa sababu yenu, kwa sababu mliendelea kujadiliana wakati ilionekana haina maana, mlikilinda mfumo unaotegemea kanuni hata mkiwa mnafanyia marekebisho, na kujenga madaraja hata yalipoporomoka.”
Chaguzi zisizowezekana
Maelezo ya kiongozi huyo wa UNCTAD yanakuja baada ya miezi ya kutokuwa na uhakika kiuchumi duniani wakati kutangazwa kuwekwa kwa ushuru kwa washirika wa kibiashara wa Marekani.
Katika maelezo yake ya hivi karibuni, Bi. Grynspan alisema kuwa kuongezeka kwa ushuru, malipo yaliyovunja rekodi ya madeni kutoka nchi zilizo na madeni makubwa na kuongezeka kwa kutokuwa na imani, yote yanazuia maendeleo.
“Nchi bado zinakabiliwa na mgogoro wa madeni, maendeleo na chaguzi zisizowezekana,” alisema. “Wanalazimika kuamua lipi deni lao au lipi maendeleo yao.”
Ushuru unaotumika na uchumi mkubwa, ikiwa ni pamoja na Marekani, umeongezeka mwaka huu kutoka wastani wa asilimia 2.8 hadi zaidi ya asilimia 20, Bi. Grynspan aliliambia hivi karibuni Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. “Kutokuwa na uhakika ndio ushuru mkubwa zaidi,” alisema, akiongeza kuwa “kunapunguza uwekezaji, kupunguza ukuaji na kufanya biashara kuwa njiangumu zaidi ya maendeleo.”
Wachuuzi wakiwa wamebeba bidhaa zao katika mpaka baina ya Rwanda na Burundi
Uwekezaji unapungua
Huko Geneva, mtaalamu mkuu wa uchumi wa UNCTAD ameonya kuwa mtiririko wa uwekezaji wa dunia unaendelea kupungua kwa mwaka wa pili mfululizo, “ukiharibu ukuaji wa kesho.”
Wakati huo huo, mfumo wa uwekezaji wa sasa unachagiza miradi katika uchumi tajiri badala ya nchi zinazoendelea, ameendelea kusema, huku gharama za mara moja zikiwa sababu ya kufanya dola moja ya Marekani “kuwa ghali mara tatu nchini Zambia kuliko huko Zurich.”
Bi. Grynspan pia amesisitiza kuwa gharama za usafirishaji sasa ni “zisizokabirika na nchi zisizo na pwani na visiwa vidogo vinavyoendelea vinapewa bili za usafirishaji hadi mara tatu ya wastani wa dunia.
Na ingawa teknolojia ya Akili Mnemba AI inatoa matarajio ya kuongeza trilioni kwa Pato la Taifa la Dunia (GDP), Katibu Mkuu wa UNCTAD ameongeza kuwa chini ya nchi moja kati ya tatu zinazoendelea zina mikakati ya kunufaika nayo. Watu bilioni 2.6 bado hawana mtandao, wengi wao ni wanawake katika nchi zinazoendelea, zinaonesha takwimu za Umoja wa Mataifa.
Madeni
Mgogoro wa madeni ya umma
Akikubaliana na wasiwasi wa Bi. Grynspan, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, ameonya kuwa madeni ya nchi zinazoendelea yalifikia dola bilioni 31 mwaka uliopita.
Hii iliashiria kuwa badala ya kuweza kuwekeza katika maisha ya wananchi wao “kwa kujenga shule zaidi au kupanua huduma za afya, serikali nyingi badala yake zinatumia fedha hizo muhimu kulipa madeni.”
Uaminifu kwa mfumo wa kimataifa pia unatia mashaka ameongeza Rais huyo wa Baraza Kuu.
Amebainisha kuwa ingawa uchumi wa dunia una thamani ya zaidi ya dola trilioni 100 kwa mwaka, mtu mmoja kati ya wawili bado “hajapanda au kuona ongezeko kidogo la mapato kwa kizazi kimoja.”