#HABARI: Wahandisi watatu na muongoza watalii mmoja wamesomewa upya mashtaka tisa ya uhujumu uchumi likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi.
Wahandisi hao ni Faustine Malya (44) Mkazi wa Salasala, Emiliani Kimaro (35) Mkazi wa Kibaha, Nelson Jacob (32) Mkazi wa Kimara Mwisho na muongoza watalii Tumaini Mollel (32) Mkazi wa jijini Mwanza.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo, baada ya kesi hiyo ya awali iliyokuwa na mashtaka nane kuondolewa na kufunguliwa nyingine mpya kwa kuongezwa kwa shtaka la kuongoza genge la uhalifu.
Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Janeth Kimango akisaidiana na
Wakili Burton Mayage mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni jijini Dar es Salaam, alidai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kwa mashtaka tisa.
Alidai kuwa mashtaka wanayoshtakiwa nayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu (4), kughushi (4) na moja ni kuongoza genge la uhalifu.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kughushi na kuongoza genge la uhalifu kati ya Novemba 5, 2021 hadi Aprili 14, 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Video kamili YouTube #ITVTANZANIA