
Dar es Salaam. Kampuni za bima za Sanlam na Allianz ambazo zimeungana na kujulikana kwa jina la SanlamAllianz imezindua soko lake rasmi nchini Tanzania.
Kampuni hizo mbili ziliungana mwaka 2023 na kuunda kampuni kubwa zaidi ya bima barani Afrika kwa upande wa huduma za kifedha zisizo za benki.
Akizungumza katika uzinduzi leo Oktoba 23, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa SanlamAllianz General Insurance Jaideep Goel, alisema kuwa muungano huo una lengo la kupanua wigo wa kutoa huduma na kuonaonyesha utekelezaji endelevu wa uanzishaji wa chapa mpya katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Goel amesema kuwa kwa sasa wanatoa huduma kwa nchi 26 barani Afrika na lengo lao ni kupenya katika nchi ambazo hazina huduma zao.
“Muungano wao pia unalenga kutumia utaalamu na uzoefu wa kimataifa hasa Pan-Afrika kufungua fursa za ukuaji katika uchumi wa uchumi katika bara la Afrika.
Kupitia muungano huu, tutawezesha vizazi kujiamini kifedha, kuwa na usalama na kustawi ikiwa pamoja na kuimarisha ujumuishaji wa fedha kwa kutoa suluhisho bunifu,” alisema.
Amesema kuwa kipaumbe chao ni kutoa suluhisho za bima za jumla zenye kuaminika na za viwango vya kimataifa ambazo zinahifadhi kile kinachowajali zaidi watu na biashara nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha SanlamAllianz, Robert Dommisse amesema kuwa muungano huo ni hatua muhimu kwa ushirikiano na sekta ya huduma za fedha nchini.
“Hii inaonyesha mkakati wetu wa kutumia utaalamu wetu katika masoko yanayokua, kuunda biashara zinazoongoza katika uchumi tunaoufanyia kazi, na pia inaunga mkono dhamira yetu ya kuwezesha watu wengi zaidi kupata huduma za fedha,” amesema.
Alifafanua kuwa kupitia ushirikiano huu, wataweza pia kuunganisha nguvu na uwezo wa kimataifa wa Sanlam na Allianz.
“Kwa fursa kubwa za usambazaji utaalamu na ushirikiano katika mawasiliano na bancassurance, tuna uhakika wateja wetu watanufaika na suluhisho bunifu za mahitaji yao,” amesema.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa SanlamAllianz bima ya maisha Julius Magabe amesema kuwa kupitia SanlamAllianz, wataleta wataalam mbalimbali wa kimataifa wenye uelewa wa utalaamu wa ndani ili kusaidia Watanzania kupanga, kulinda, na kustawi.
“Kipaumbele chetu kitakuwa kwenye bidhaa bunifu za bima ya maisha zinazochangia usalama wa fedha wa muda mrefu na ujumuishaji wa fedha,” amesema.