“Watu wa Gaza wamepitia mateso yasiyoweza kuelezeka, wanahitaji msaada unaowafikia haraka na kwa usalama, kupitia njia na vituo vyote vinavyowezekana. Makazi si anasa, ndiyo yanayowawezesha familia kupumzika, kukaa katika joto, na kuanza kujenga upya maisha yao. Bila makazi, uokoaji hauwezi kuanza. Kila mtu anastahili kuishi kwa usalama na utu, na msaada wa kibinadamu, ikiwemo chakula, maji, dawa na makazi lazima ufikishwe kwa kila mtu, kila mahali.” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope.
Baada ya miezi kadhaa ya kuhama, Maha anapokea hema ya kumhifadhi yeye na watoto wake.
Mahitaji ya makazi bado ni makubwa, huku asilimia 90 ya wakazi wakikadiriwa kuwa wamehamishwa. Kwa mujibu wa kikundi cha Shelter Cluster, angalau watu milioni 1.5 wanahitaji kwa dharura msaada wa makazi ya muda, huku vifaa vilivyopo vikiwa karibu kuisha kabisa.
Maelfu ya watu wanarudi taratibu makwao, lakini wanakuta nyumba zao zikiwa vifusi na miundombinu ya msingi ikiwa imeharibiwa. Kwa ukosefu wa hema au turubai, wengine wanatumia mabegi ya unga na mchele kujikinga na upepo na mvua.
IOM imeweka tayari mamilioni ya vifaa vya uokoaji kwa ajili ya usafirishaji wa haraka, vikiwemo zaidi ya hema 28,000 vilivyohifadhiwa Jordan kwa ajili ya watu hadi 168,000, pamoja na blanketi, magodoro, na vifaa vya usafi. Zaidi ya vifaa milioni 4.1 vya maandalizi ya msimu wa baridi, vikiwemo turubai na taa za jua, pia viko tayari kusafirishwa ili kuboresha hali ya maisha katika makazi yaliyoathirika au yenye msongamano.
Licha ya usitishaji mapigano, vikwazo vya kiutawala kama ucheleweshaji wa forodha, idadi ndogo ya vituo vya mipakani, na hali tete ya usalama bado vinazuia utoaji wa misaada. IOM ipo tayari kujibu haraka na kwa wigo mpana, mradi tu ruhusa kamili, salama, na isiyo na vizuizi ya kibinadamu itolewe na mamlaka husika za Israeli, kwa mujibu wa kanuni za kibinadamu.
Baada ya miezi kadhaa ya kuhama, Maha na watoto wake wanapokea vifaa vya kuokoa maisha, lakini maelfu ya wengine wanasalia kunyimwa.
Baada ya kuzuiliwa kabisa kwa miezi sita kwa vifaa vya makazi, mahitaji kote Gaza bado ni makubwa. Tangu tangazo la usitishaji mapigano, IOM imeanza kutoa msaada muhimu, lakini bado inahitajika zaidi ili kukidhi mahitaji ya dharura ya watu milioni 1.5 wasio na makazi salama. Familia zisizo na makazi zinakabiliwa na hatari kubwa za magonjwa, njaa, na ukatili.
Kati ya misaada iliyowasili karibuni, mahema 2,500 yaliyosafirishwa wiki iliyopita yatazigawiwa na washirika wa kibinadamu kwa angalau watu 15,000 waliokosa makazi kote Gaza, yakitoa hifadhi dhidi ya hali ya hewa inayoendelea kuwa baridi zaidi. Hema hizo zilitolewa na Umoja wa Ulaya na Irish Aid, na zikapelekwa Gaza kwa uratibu na Kikundi cha Usafirishaji wa Misaada ya Kibinadamu.