Tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Dunia wa Kutokomeza Polio mwaka 1988, wagonjwa wa polio duniani wamepungua kwa zaidi ya asilimia 99.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi amesema wakati mpango huo ulipoanza, zaidi ya watoto 350,000 walikuwa wanapata kupooza kila mwaka kutokana na polio. Mwaka huu 2025, hadi sasa, ni wagonjwa 36 pekee waliopata maambukizi ya virusi vya polio wameripotiwa duniani.

“Ufanisi huu umetokana na juhudi za muda mrefu za washirika wetu, hususan Rotary International ambao walikuwa waasisi wa jitihada hizi,” amesema Dkt. Tedros. “Lakini kazi haijaisha. Mradi polio ipo sehemu yoyote duniani, watoto wote wako hatarini. Miaka iliyopita dunia iliweza kushinda vikwazo vya kisiasa na kijiografia kutokomeza ndui; sasa tunapaswa kukamilisha hatua ya mwisho ya kutokomeza polio.”

Ugonjwa wa Polio

Polio, kitaalamu ikijulikana kama poliomyelitis, ni ugonjwa wa virusi unaoambukiza kwa urahisi na hushambulia mfumo wa neva, na unaweza kusababisha kupooza kabisa ndani ya saa chache.

Ugonjwa huu huathiri zaidi watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, lakini mtu yeyote ambaye hajachanjwa anaweza kuambukizwa.

Kwa sasa hakuna tiba maalum ya polio, bali njia pekee ya kujikinga ni kupitia chanjo za mara kwa mara zinazotoa kinga ya kudumu.

Juhudi ziendelee

Kwa sasa, maeneo machache tu duniani bado yana maambukizi ya virusi vya polio.

WHO inahimiza nchi zote kuendelea kuwekeza kisiasa na kifedha, na kuunganisha mifumo ya ufuatiliaji, majibu ya dharura na uhamasishaji wa jamii iliyoanzishwa na miradi ya polio katika mifumo ya afya kwa ujumla. Hatua hii itasaidia kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na changamoto za kiafya zijazo.

WHO inahimiza nchi wanachama na wadau kuendelea kuwekeza kwa dhati kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo zinazookoa maisha.

Je ungependa kujua juhudi zinazofanyika katika nchi mbalimbali kwenye kupambana na ugonjwa huu? Bofya hapa kujua kuhusu nchi ya Cameroon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *