Akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa 15 wa ASEAN na Umoja wa Mataifa mjini Kuala Lumpur, Malaysia hii leo Jumatatu Oktoba 27, Guterres amesema kuwa hali nchini Myanmar “imegeuka kuwa janga la kibinadamu na kisiasa,” akilaani mauaji, mashambulizi ya anga kwa raia na ukosefu wa uwajibikaji unaoendelea tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.
“Jeshi linashambulia raia ambao linapaswa kuwalinda. Maelfu wameuawa, mamilioni wamekimbia makazi yao, na vijiji vimechomwa moto. Lazima ghasia hizi zikome mara moja,” amesema Guterres.
Mwanamke akiwa amembeba mtoto wake wa kiume mwenye umri wa wa mwaka 1 wakati wa kutembelea kituo cha lishe cha UNICEF katika kambi ya wakimbizi ya Rohingya huko Cox’s Bazar, Bangladesh.
Ushirikiano wa ASEAN na Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu amesifu jukumu la ASEAN kama mshirika muhimu wa Umoja wa Mataifa katika kulinda amani, haki za binadamu na ustawi wa kikanda. Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu Makubaliano ya Vipengele Vitano – makubaliano ambayo yanalenga kumaliza mgogoro wa Myanmar kupitia mazungumzo jumuishi, usitishaji wa mapigano, na uanzishaji wa serikali ya kiraia.
“Tunapongeza juhudi za ASEAN katika kuimarisha ushirikiano na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, Julie Bishop, na katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Myanmar. Watu wa Myanmar wanahitaji msaada wetu wa pamoja – hebu tuitikie wito huo,” amesisitiza.
Guterres pia amesisitiza kuwa juhudi za ASEAN katika kudhibiti migogoro mingine, ikiwemo mazungumzo ya Kanuni za Vitendo katika Bahari ya Kusini ya China, zinaonesha uwezo wa kanda hiyo kuwa mfano wa amani na diplomasia duniani.
Wito wa kurejesha demokrasia na utawala wa sheria
Katibu Mkuu ametoa wito wa wazi kwa viongozi wa kijeshi nchini Myanmar kuachia mamlaka na kuruhusu kurejea kwa demokrasia. Ametaka kuachiwa mara moja kwa wafungwa wote wa kisiasa, kuanzishwa kwa mazungumzo jumuishi yanayoshirikisha makundi yote, na kufunguliwa kwa njia salama za misaada ya kibinadamu.
“Mwelekeo sasa ni kurejesha taasisi za kidemokrasia zinazoongozwa na sheria na haki za binadamu. Hii lazima ijumuishe watu wote – wakiwemo waislamu wa kabila la warohingya, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyimwa haki na matumaini ya amani,” amesema Guterres.
Ameongeza kuwa mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika mwezi uliopita mjini New York nchini Marekani, umeonesha upya dhamira ya kimataifa kusaidia jamii ya warohingya na nchi zinazowapokea wakimbizi hao, akitaka misaada hiyo iende sambamba na hatua za kisiasa za kudumu.
Katibu Mkuu Antonio Guterres (kushoto) akilakiwa na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim wa Malaysia katika ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa wakuu wa ASEAN kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kuala Lumpur.
Amani na usalama wa kikanda
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, kuendelea kwa machafuko nchini Myanmar kunahatarisha uthabiti wa kanda yote. Ameonya kwamba mgogoro huo unaongeza uhalifu wa kuvuka mipaka, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya, pamoja na wimbi la wakimbizi katika nchi jirani.
“Hali ya Myanmar ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa kikanda. ASEAN na Umoja wa Mataifa lazima ziendelee kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha amani inarejea, raia wanalindwa na sheria za kimataifa zinaheshimiwa,” amesema.
Umoja wa Mataifa na ASEAN – washirika wa amani
Guterres amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa ASEAN katika kudumisha amani, maendeleo na haki za binadamu katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia.
“ASEAN inaweza kuwa taa ya matumaini katika nyakati hizi zenye giza. Umoja wa Mataifa unasimama bega kwa bega na ASEAN kuhakikisha mustakabali wa amani, haki na ustawi kwa watu wa kanda hii na dunia nzima,” amesema Katibu Mkuu.