Tume ya Umoja wa Afrika imeelezea wasiwasi wake kuhusu kauli za hivi karibuni za Marekani, ambazo zimeituhumu serikali ya Nigeria kuwa inashiriki katika mauaji iliyodai kuwa yanayowalenga Wakristo, na kudokeza uwezekano wa kuingilia kijeshi kwa kisingizio cha “kutetea uhuru wa kidini.”
Taarifa rasmi ya Tume ya Umoja wa Afrika imesisitiza kushikamana kwake kwa dhati na kanuni za mamlaka ya kujitawa na kutoingilia mambo ya nchi nyingine, uhuru wa kidini na utawala wa sheria, kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Umoja wa Afrika na vyombo vinavyohusiana.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba Jamhuri ya Shirikisho ya Nigeria ni nchi mwanachama muhimu wa taasisi hiyo, yenye nafasi muhimu katika kulinda utulivu wa kikanda, kupambana na ugaidi, ulinzi wa amani na ustawi wa bara.
Umoja wa Afrika umesisitiza udharura wa kuheshimiwa mamlaka ya Nigeria katika kusimamia mambo yake ya ndani, ikiwa ni pamoja na usalama na haki za binadamu, kwa mujibu wa katiba yake na majukumu ya kimataifa.
Taarifa ya Umoja wa Afrika imetolewa baada ya matamshi ya vitisho ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alidokeza uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Abuja, akiituhumu serikali ya Nigeria kuwa imezembea kuwalinda Wakristo. Matamshi hayo ya vitisho ya Trump yamekosolewa sana ndani na nje ya Afrika, huku kukitolewa maonyo kuhusu athari za kauli kama hizo kwa usalama wa kikanda.

Umoja wa Afrika umeeleza kuwa Nigeria inakabiliwa na changamoto ngumu za usalama zinazowaathiri raia wake wenye imani na dini mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukatili unaofanywa na makundi yenye msimamo mkali, ujambazi, migogoro ya kidini na mizozo kuhusu rasilimali, ukitoa wito wa kuwepo ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuunga mkono uwezo wa nchi hiyo wa kukabiliana na changamoto hizo, kuwalinda raia wote, kukuza haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika wa ukatili.