Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba walowezi wa Israel wamefanya mashambulizi yasiyopungua 264 dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu mwezi uliopita wa Oktoba, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya kila mwezi tangu maafisa wa Umoja wa Mataifa walipoanza kufuatilia mashambulizi kama hayo mwaka 2006.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya katika taarifa yake kuhusu ongezeko kubwa la kasi ya ukatili, ikisema kwamba mashambulizi hayo, ambayo yamesababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali, yalikuwa wastani wa matukio 8 kwa siku.
Ofisi hiyo imesema, “Tangu mwaka 2006, tumerekodi zaidi ya mashambulizi 9,600 ya aina hii dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi. Takriban 1,500 kati yao yametokea mwaka huu pekee, ambayo ni takriban 15% ya jumla ya mashambulizi yote.”

Ukingo wa Magharibi, wenye Wapalestina wapatao milioni 2.7, ni kitovu kikuu cha juhudi za kuanzisha taifa huru la Palestina, lakini serikali mtawalia za Israel zimepanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa kasi kubwa katika eneo hiilo na kuligawa vipandevipande.
Umoja wa Mataifa, Wapalestina, na nchi nyingi duniani zinavitambua vitongoji hivyo kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.
Zaidi ya walowezi nusu milioni wa Israel wanaishi katika ardhi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataiifa imesema data zake zinaonyesha kuwa watoto 42 wa Kipalestina wameuawa na askari wa Israel katika Ukingo wa Magharibi tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi Jumatano wiki hii.