Fountain Gate FC imetawala Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kunyakua tuzo tatu tofauti za mwezi huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo, tuzo ambazo Fountain Gate imezinyakua za mwezi Oktoba ni Kocha Bora wa Ligi Kuu, Mchezaji Bora wa Ligi Kuu na Meneja Bora wa Uwanja.

Tuzo ya Mchezaji Bora imechukuliwa na Issa Abushiri huku Mohamed Laizer akitwaa ya Kocha Bora na Meneja Bora wa Uwanja ni Jackson Mwendwa.

“Abushiri alitoa mchango mkubwa kwa timu yake kupata ushindi katika michezo miwili iliyocheza na sare katika mchezo mmoja ambapo alifunga bao moja. Fountain Gate ilishinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na ikashinda bao 1-0 dhidi ya KMC FC, na sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union.

“Kwa upande wa Laizer aliwashinda Zedekia Otieno wa Tanzania Prisons na Francis Baraza wa Pamba Jiji alioingia nao fainali katika mchakato huo. Aliiongoza Fountain Gate katika michezo mitatu na kujikusanyia alama saba, ikiwa na jumla ya mabao mawili ya kufunga na haijaruhusu bao. Laizer ameisaidia pia timu kutoka kwenye nafasi ya 14 hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo,” imefafanua taarifa ya TPLB.

Wakati huohuo Kamati ya Tuzo za TFF,imemchagua Rishedy Kihedu wa Mbuni FC kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba wa Ligi Championship ya NBC 2025/26, huku Leonard Budeba pia wa Mbuni FC akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Kihedu aliyeingia fainali katika mchakato huo na Naku James wa Polisi Tanzania pamoja na Kilaza Mazoea wa Geita Gold, alionesha kiwango chenye mwendelezo, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu katika michezo mitatu ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo.

Kwa upande wa Budeba aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Geita Gold na Mbwana Makata wa Polisi Tanzania, aliiongoza Mbuni kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *