Bundi wa majeraha ameanza kulia katika Kambi ya Timu ya Taifa ya England inayojiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia baadaye mwezi baada ya nyota wawili wa Newcastle United kulazimika kurudishwa klabuni baada ya kupata majeraha.
Wachezaji hao ni Anthony Gordon na Nick Pope na tayari benchi la ufundi la England limeshaita wachezaji wa kuziba nafasi zao.
Gordon ambaye alikosekana katika mchezo wa Ligi Kuu England (EPL) wa Newcastle United baada ya kupata maumivu ya paja na Pope alilazimika kutolewa katika mchezo huo baada ya kugongana kichwani.
Meneja wa Newcastle United, Eddie Howe alionyesha wasiwasi wa kukosekana kwa wachezaji hao katika mechi mbili zijazo za England na hatimaye Chama cha Mpira wa Miguu cha nchi hiyo kimethibitisha rasmi kuwa wameenguliwa kikosini.
Kukosekana kwa Gordon na Pope kumefungua milango kwa Beki wa Chelsea, Trevoh Chalobah pamoja na kipa wa Manchester City, James Trafford kuingia kikosini.
Kuna wasiwasi pia wa kukosekana kwa Marc Guehi ambaye alikosa mchezo uliopita wa Crystal Palace dhidi ya Brighton ingawa beki huyo tayari ameanza mazoezi akiwa na kikosi cha timu hiyo ya taifa iliyo chini ya Thomas Tuchel.
Meneja wa Crystal Palace, Oliver Glasner alisema kuwa Guehi ‘hawezi hata kutembea’, lakini benchi la ufundi la England linaendelea kujiridhisha juu ya hali yake kisha kuamua kama limtumie au lisimtumie.
Hata hivyo presha inaonekana sio kubwa sana kwa vile michezo hiyo niya kukamilisha tu ratiba kwa England kwani tayari imeshafuzu Fainali za Kombe la Dunia kupitia kundi K baada ya kufikisha pointi 18 mwezi uliopita.
Alhamisi, Novemba 13, 2025, England itakuwa nyumbani kuikaribisha Serbia na Novemba 16, 2025 itakuwa ugenini kucheza na Albania.