
Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) limetaka kuchukuliwa hatua za haraka ili kuwasaidia mamilioni ya raia walioathiriwa na vita vya Sudan kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Amy Pope, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la IOM alisema hayo baada ya kuwasili Sudan jana kwa lengo la kutathmini misaada ya kibinadamu katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.
Pope ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuwasaidia mamilioni ya watu walioathiriwa na mgogoro huko Sudan.
Ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada, Karibu watu milioni 10 wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi.
Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF wanapigana vita tangu Aprili 15, 2023, vita ambavyo vimeshindwa kuhitimishwa kupitia upatanishi wa kikanda na kimataifa. Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mgogoro wa Sudan.
Mashirika ya ndani ya Sudan na ya kimataifa yanasema kuwa hali ya mambo ilizidi kuwa mbaya mwishoni mwa mwezi uliopita wakati kikosi cha RSF kilipouteka mji wa El-Fasher ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na kufanya mauaji ya halaiki ya kikabila.
Wakati huo huo, kamati ya dharura ya misaada katika mji wa Tawila huko Darfur Kaskazini imeeleza kuwa moto uliibuka mashariki mwa kambi ya Dali na kuangamiza mali za raia wakimbizi.
Kamati hiyo imezitolea wito taasisi za masuala ya kibinadamu kuzisaidia haraka familia zilizoathiriwa na moto.
Darfur inaunda takriban moja ya tano ya ardhi ya Sudan.