Mapigano kati ya makundi hasimu ya kigaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria yamesababisha vifo vya magaidi wasiopungua 200 katika eneo la Ziwa Chad.

Duru za kijeshi na kiitelijinsia za Nigeria zimeripoti kuwa mapigano kati ya kundi la Boko Haram na mahasimu wao wa kundi la ISWAP lenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) yalijiri siku ya Jumapili huko Dogon Chiku katika eneo la Ziwa Chad.

Duru hizo zimearifu kuwa magaidi wa kundi la ISWAP wasiopungua 200 wameuawa katika mapigano hayo na kundi la Boko Haram. 

Mkazi wa kaskazini mashariki mwa Nigeria anayefuatilia kwa karibu ghasia zinazoendelea katika eneo hilo ameeleza kuwa magaidi wa ISWAP wasiopungua 200 wameuawa katika mapigano hayo na silaha zao kadhaa zimenaswa. 

Kundi la Boko Haram limepoteza wanachama wake wanne katika mapigano na kundi hasimu la ISWAP. 

Naye mkazi wa jimbo la Borno aliyefahamika kwa jina la Saddiku amesema mapigano hayo ya Jumapili kati ya Boko Haram na ISWAP yanaweza kuwa mzozo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya makundi hayo mawili nchini Nigeria tangu yaanza kushambuliana. 

Duru ya kiintelijinsia ya Nigeria pia imeripoti kuwa wanafuatilia taathira za mapigano hayo ambayo imesema kuna taarifa kuhusu mapigano hayo ambayo ni habari njema. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa makundi ya ISWAP na Boko Haram yamekuwa yakipigana vikali yakigombania udhibiti wa ardhi tangu makundi hayo yagawanyike mwaka 2016 kutokana na tofauti za kiitikadi, huku mapigano mengi yakifanyika karibu na eneo la Ziwa Chad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *