Kenya inatazamia kutimua uwezo wa bandari ya Chabahar ya Iran na kama kitovu cha kanda kwa ajili ya uagizaji na usambazaji wa chai na kahawa.

Hayo yamebainika katika kikao kilichofanyika kati ya Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa Eneo Huru la Chabahar, pamoja na Jonah Maina Mwangi, Balozi wa Kenya mjini Tehran.

Wamejadili uwezo wa bandari ya Chabahar na miundombinu yake ya usafirishaji kama kitovu cha kanda kwa ajili ya uagizaji na usambazaji wa chai na kahawa. Pande zote mbili zilitilia mkazo nafasi ya kipekee ya kijiografia ya Chabahar na uwezo wa uzalishaji wa Kenya, huku wakihimiza kuendelezwa kwa mahusiano ya kibiashara na uwekezaji wa pamoja.

Aidha wamechambua fursa za ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika sekta ya biashara ya kilimo, hususan chai na kahawa. Kikao hicho kilifanyika kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kutumia nafasi ya kijiografia ya Chabahar kusambaza bidhaa za Afrika katika masoko ya Asia.

Bw. Arbabi alisisitiza kuwa Chabahar, ikiwa ni bandari pekee ya Iran iliyo kwenye Bahari ya Hindi, ina uwezo wa kuwa kitovu cha kikanda cha uagizaji na usambazaji wa chai na kahawa kutoka Kenya. Bandari hiyo ina njia ya moja kwa moja kuelekea nchi za Asia ya Kati, Afghanistan na hata Asia ya Kaskazini, na hivyo ina uwezo mkubwa wa kusafirisha bidhaa za kilimo.

Ameongeza kuwa, kutokana na miundombinu inayokua kwa kasi katika Eneo Huru la Chabahar, ikiwemo maghala maalum, njia za usafirishaji wa kimataifa, na msamaha wa kodi, inawezekana kuunda mnyororo thabiti wa usambazaji wa bidhaa kutoka Kenya. Ushirikiano huu unaweza kusaidia kuongeza mauzo ya nje ya Kenya na kuifanya Iran kuwa kituo kikuu cha biashara ya chai na kahawa katika ukanda huu.

Kwa upande wake, Balozi wa Kenya alieleza kufurahishwa na uwezo wa kiuchumi wa Iran, na akasisitiza haja ya kuendeleza mahusiano ya kibiashara na uwekezaji wa pamoja. Alisema kuwa Kenya ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chai na kahawa barani Afrika, na Iran, kwa kuwa na idadi kubwa ya watumiaji na nafasi nzuri ya usafirishaji, ni mshirika bora wa kupanua masoko ya Kenya barani Asia.

Aidha, alisisitiza utayari wa sekta binafsi ya Kenya kushiriki katika miradi ya pamoja huko Chabahar, na akaongeza kuwa kwa kurahisisha taratibu za forodha na kuanzisha njia za moja kwa moja za usafirishaji, mauzo ya bidhaa za kilimo kutoka Kenya yanaweza kuongezeka kwa kiwango kikubwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *