
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa le na msemaji wa IOM kwa vyombo vya habari mjini Geneva, tukio hilo linaongeza idadi ya vifo katika bahari ya Mediterania ya Kati, ambayo sasa imevuka idadi ya vifo 1,000 tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2025.
“Tunatuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha katika ajali hii ya kusikitisha,” amesema msemaji huyo wa IOM. “Tukio hili ni ukumbusho mwingine wa gharama kubwa ya kukosa njia salama na halali za uhamiaji. Ni lazima hatua za pamoja zichukuliwe mara moja kuokoa maisha.”
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka za Libya, ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe 8 mwezi Novemba, wakati boti hiyo ilipopinduka karibu na Kiwanda cha Mafuta cha Al Buri. Operesheni ya uokoaji ilianzishwa mara moja, kwa ushirikiano na timu ya IOM.
Waliokuwemo ndani ya boti
Ripoti za IOM za manusura zinaeleza kuwa boti hiyo, iliyokuwa imebeba idadi ya wahamiaji 49 wakiwemo wanaume 47 na wanawake 2, iliondoka Zuwara, mji wa Pwani ya bahari ya Mediterania magharibi mwa Libya, mnamo tarehe 3 mwezi Novemba, saa tatu usiku saa za Lybia.
Baada ya takribani saa sita, mawimbi makubwa yaliharibu injini na kusababisha boti kupinduka, huku abiria wote wakitupwa baharini.
Baada ya kutangatanga kwa siku sita baharini, wanaume saba pekee waliokolewa wakiwa hai wakiwemo wanne kutoka nchi ya Sudan, wawili kutoka Nigeria, na mmoja kutoka nchini Cameroon.
Hata hivyo, watu 42 bado hawajapatikana na wanahofiwa kufa maji, wakiwemo 29 kutoka Sudan, wanane kutoka nchini Somalia, watatu kutoka Cameroon, na wawili kutoka nchini Nigeria.
Timu ya IOM imewapatia manusura huduma ya kwanza ya matibabu, chakula, na maji walipowasili katika kituo cha kutia nanga kwa ushirikiano na mamlaka husika.
“Hii siyo ajali ya kwanza mwaka huu, na inaonesha hatari kubwa inayowakabili wahamiaji wanaotumia Njia ya Kati ya Bahari ya Mediterania,” ameongeza msemaji wa IOM. “Tunatoa wito kwa serikali zote katika ukanda huu kuimarisha juhudi za utafutaji na uokoaji, na zaidi ya yote, kupanua njia salama za uhamiaji ili kuzuia vifo visivyo vya lazima.”
Tukio hili linajiri wiki chache tu baada ya ajali nyingine mbaya zilizotokea karibu na Surman na Lampedusa, visiwa vilivyopo kwenye bahari hiyo ya Mediterania, likiongeza shinikizo kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti.
Kwa mujibu wa Programu ya Watu Waliopotea ya IOM, zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha katika safari za kuvuka bahari ya Mediterania mwaka 2025 pekee. Kwa tukio hili jipya, idadi hiyo imeongezeka zaidi, ikiweka wazi haja ya hatua za haraka katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
“Kila maisha yaliyopotea ni kumbusho la wajibu wetu wa pamoja, hakuna mtu anayepaswa kufa akiwa anatafuta maisha bora.”