
“Homa ya mapafu bado inaua watoto wengi kuliko ugonjwa mwingine wowote wa kuambukiza,” imesema WHO katika taarifa yake kutoka Geneva iliyotolewa leo.
Shirika hilo limeongeza kuwa homa hiyo “Bado ni tishio kubwa hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambako upatikanaji wa chanjo, uchunguzi, na tiba ya hewa ya oksijeni ni mdogo.”
Mifumo ya afya iimarishwe
WHO imesisitiza kuwa kuwalinda watoto na jamii dhidi ya homa ya mapafu kunahitaji kuimarisha mifumo ya afya, ili hatua za kinga ziwafikie wote na kila mtu mwenye dalili apate uchunguzi wa haraka na matibabu sahihi, ikiwemo dawa za antibiotic na oksijeni ya kitabibu inapohitajika.
Shirika hilo limeeleza kuwa “Tunajua nini kinafanya kazi. Kuchukua hatua za haraka kutahakikisha kila pumzi ina maana.”
Kwa mujibu wa WHO, njia mojawapo muhimu za kupunguza vifo ni kuongeza hatua za kinga, ikiwemo kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo muhimu dhidi ya Haemophilus influenzae aina ya b (Hib), pneumococcus, surua, na kifaduro.
Shirika hilo pia limehimiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, lishe bora, na mazingira yasiyo na moshi wa tumbaku wala uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba vinasaidia kuwalinda watoto.
Huduma za afya ya msingi ni muhimu
WHO imeongeza kuwa ni muhimu kuimarisha huduma za afya ya msingi, kwa kuwapatia wahudumu wa afya vifaa na mafunzo ya kutambua na kutibu nimonia mapema.
“Wahudumu wa afya lazima wawezeshwe kwa maarifa, vifaa vya uchunguzi, na rasilimali wanazohitaji kuokoa maisha,” limesema shirika hilo.
Aidha, WHO imesisitiza umuhimu wa usawa na uwajibikaji katika kukabiliana na homa ya mapafu “Ni lazima tuzibe pengo la upatikanaji wa chanjo, oksijeni na huduma za afya,” limesisitiza, likizitaka nchi kuunganisha udhibiti wa homa ya mapafu katika programu pana za afya ya mtoto, wazee, na afya ya mazingira.
Upatikanaji wa hewa ya oksijeni ni muhimu
Shirika hilo pia limezitaka serikali na washirika kuongeza upatikanaji wa hewa ya oksijeni ya kitabibu, likisema hakuna kituo cha afya kinachopaswa kukosa rasilimali hii muhimu.
“Kila hospitali na zahanati inapaswa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa hewa ya oksijeni, vipimo vya pulse oximeter, na wafanyakazi waliopatiwa mafunzo ya matumizi salama ya vifaa hivyo,” WHO imesisitiza
Katika kuadhimisha Siku ya Homa ya Mapafu Duniani kwa kaulimbiu “Kila Pumzi Inamaana,” WHO imerejelea dhamira yake ya kuunga mkono nchi katika kuimarisha kinga na matibabu ya homa ya mapafu ili kuhakikisha hakuna mtu anayepoteza maisha kwa ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika.