Katika barua rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amelaani Marekani kwa jukumu lake katika kuunga mkono uchokozi wa kijeshi wa Israeli dhidi ya Iran mnamo Juni, kufuatia kauli za Rais Donald Trump akithibitisha usimamizi wa Marekani juu ya mashambulizi hayo.

Barua ya Araghchi, iliyowasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, ilinukuu kauli ya Trump ya Novemba 6, ambapo alisema: “Israel ilishambulia [Iran] kwanza. Shambulio hilo lilikuwa kali sana. Nilikuwa na usimamizi kamili juu yake.”

Mwanadiplomsia huyo wa ngazi ya juu alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kauli hiyo ni ushahidi dhahiri wa uelekezi na usimamizi wa Marekani juu ya mashambulizi ya kijeshi yaliyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Iran.

Barua hiyo ilirejelea mawasiliano ya awali yaliyotumwa na Jamhuri ya Kiislamu kwa Baraza la Usalama mnamo Juni 13, 22 na 28, ambapo Tehran vilevile ilipinga “vitendo vya wazi vya uchokozi” vilivyofanywa na Washington na Tel Aviv kati ya Juni 13 hadi 24 dhidi ya ardhi ya Iran.

Araghchi amesema mashambulizi hayo yalilenga raia wa Iran, miundombinu na vituo, ikiwemo maeneo ya nyuklia ya amani yaliyokuwa chini ya uangalizi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), na kusababisha kuuawa shahidi zaidi ya watu 1,100 na kujeruhi wengine wengi.

Amesisitiza kuwa mashambulizi hayo yalikiuka mifumo kadhaa ya kisheria ya kimataifa.

Alieleza kuwa jukumu la ukiukaji huu linabebwa si tu na utawala wa Israel, bali pia na Marekani, ambayo, kwa mujibu wa kukiri kwa Trump, iliendesha na kudhibiti uchokozi huo wa Israel.

Barua ya Araghchi imeitaka Marekani kutoa fidia kamili kwa hasara zilizotokana na mashambulizi hayo.

Barua hiyo pia ilibainisha kuwa uwajibikaji unawahusu pia maafisa wa Israel waliotoa amri, maagizo au kusaidia katika uhalifu wa kivita.

Araghchi alihitimisha kwa kuhimiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kuchukua hatua stahiki kuhakikisha uwajibikaji wa Marekani na utawala wa Israel, akisisitiza haja ya kuwasilisha wahusika wa uhalifu huu mbele ya vyombo vya sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *