
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo Ijumaa, litapiga kura katika kikao maalumu kinachojadili mgogoro wa Sudan, kuhusu rasimu ya azimio linalolaani ukiukwaji wa haki za binadamu ambao linasema umefanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ndani na karibu na mji wa El Fasher katika shambulio la hivi karibuni la wapiganaji wa kundi hilo dhidi ya mjini huo.
Rasimu ya azimio hilo inalaani kile inachokielezea kama ukatili mkubwa ulioripotiwa kufanyika, ikiwa ni pamoja na mauaji yanayochochewa na ukabila, mateso, mauaji ya papo na hapo, kukamatwa watu kiholela, ubakaji na mengineyo.
Baraza hilo pia linautaka ujumbe wa kutafuta ukweli kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu ukiukwaji huo wa haki za binadamu ndani na karibu na mji wa El Fasher, na kubaini wale wanaoaminika kuhusika na ukiukwaji huo.
Rasimu ya azimio hilo inalaani aina zote za uingiliaji kati wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan, ambao inasema unachochea mzozo huo, na inazitaka pande zote, za ndani na nje, kuheshimu umoja na mamlaka ya kujitawala ya Sudan.
Pia inatoa wito wa kurahisisha upatikanaji wa haraka na bila vikwazo wa misaada ya kibinadamu, na kuhakikisha ulinzi wa raia chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu wale wanaotaka kuondoka El Fasher kufanya hivyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki mjini El Fasher, pamoja na kuongezeka mapigano katika maeneo ya Kordofan.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssef huko New York, Guterres alitoa wito kwa jeshi la Sudan na kundi la waasi la RSF kushiriki katika mchakato wa mazungumzo ya haraka na mjumbe wake maalumu.