Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema vyombo vya kidiplomasia vinapaswa kumfungulia mashtaka Donald Trump mhalifu katika majukwaa ya kimataifa.

Akiashiria hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kukiri kwamba alisimamia mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema: “Trump amesema waziwazi kwamba aliongoza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Katika suala hili, taasisi ya diplomasia imetoa taarifa ya kulaani jambo hilo. Japokuwa baada ya kukiri huko hakuna hatua inayochukuliwa na jumuiya za kimataifa, lakini hatuna chaguo ila kuwasilisha mashtaka. Kwa hivyo, naomba taasisi ya diplomasia iwasilishe mashtaka dhidi Trump mtendajinai.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa ya leo, Sayyid Khatami ameihimiza serikali kushughulikia kero na matatizo ya kimaisiha ya wananchi hususan suala la mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali.

Vilevile amezungumzia suala la vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, na kusema: Hijabu ni suala la kidini na kisheria. Amewahimiza wanawake wa Kiislamu kuiga nyayo za Bibi Fatimatu Zahraa, binti kipenzi wa Mtume Muhammad (SAW) na Mbora wa Wanawake wa Peponi katika kuvaa vazi la staha la hijabu.  

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran pia amezungumzia kupungua kwa mvua na maji na kusema: “Hali hii haijawahi kutokea nchini Iran katika kipindi cha miaka 57 iliyopita. Tatizo hili si la Iran pekee bali ni tatizo la kimataifa, na Swala za maombi ya mvua zinafanyika katika nchi za Kiislamu ikiwemo Iran.”

Amesema: “Imeelezwa katika Hadithi kwamba dhambi zina taathira katika kutokea mambo kama haya, kwa hivyo ni lazima turejee kwa Mwenyezi Mungu na kushiriki katika Swala za kuomba mvua kwa ikhlasi.”

Amewahimiza wananchi kuacha israfu na ufujaji na kuamrisha mema na kukatazana maovu. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *