Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali itafanya uwekezaji mkubwa wa michezo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hilo limeahidiwa leo na Rais Samia wakati akihutubia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mheshimiwa Spika; Michezo ni uchumi. Hatuwezi kupata matokeo makubwa bila kuwekeza. Miongoni mwa hatua tutakazozichukua ni kuanzisha na kuendeleza shule za michezo (sports academies) kwa lengo la kuwaandaa wanamichezo wa leo na kesho,” amesema Rais Samia.

Rais amesisitiza pia kuwa kipaumbele kingine kikubwa cha nchi katika miaka mitano ijayo ni uandaaji mzuri wa Fainali za AFCON 2027.

“Kama mnavyofahamu, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON

mwaka 2027, na kuelekea huko tutakamilisha ujenzi wa viwanja vitakavyotumika, ikiwemo

Uwanja wa AFCON uliopo Arusha, na maboresho ya viwanja vingine nchini.

“Vilevile, tutaendelea kuvutia michezo mbalimbali kufanyika hapa nchini ili kuongeza fursa zitokanazo na kuwa mwenyeji wa michezo hiyo,” amesema Rais Samia.

Rais wa CAF, Patrice Motsepe, Jumatatu, Septemba 27, 2023 alitangaza  rasmi ushindi wa maombi hayo ya nchi hizo tatu zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo ambacho wajumbe wake 22 walipiga kura ya kuchagua mshindi kati ya tenda nne zilizowasilishwa mezani.

Motsepe alisema kuwa kilichobeba maombi ya pamoja ya Tanzania, Kenya na Uganda mbali na utayari huo wa marais wa nchi husika ambao ni Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Yoweri Museven (Uganda) na William Ruto wa Kenya ni urahisi wa usafiri wa watu kutoka eneo moja hadi lingine, uhakika wa miundombinu na pamoja na ukarimu wa watu wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *