Dar es Salaam. Mwigizaji na Mwongozaji wa filamu za Bongo, Mahsein Awadhi ‘Dk Cheni’ amefichua siri ya ndoa yake kudumu kwa miaka 17 sasa, huku akitaja mapenzi kwa mkewe na mambo mengi yameifanya izidi kustawi na hajui kitu kurogwa.

Akizungumza na Mwananchi, Cheni ambaye anatamba na filamu na tamthilia nyingi Bongo, amesema watu wengi ndoa zao zinayumba kwa sababu ya namna wanavyoishi, tofauti na yeye ambaye amekuwa msaada mkubwa kwake na hasa kazi za nyumbani.

Amesema katika ndoa yake, anajiona mshindi kwani mbali na mapenzi anayopata kwa mkewe, pia ni pambo na anahitaji kusaidiwa, naye anatekeleza mambo yote muhimu kwake.

“Mwanamke ni kama pambo, hili wanaume wengi hawalitambui,” amesema na kuongeza; 

“Kuna baadhi ya kazi ambazo wanawake wanafanya, lakini hawakupaswa kabisa kuzifanya.”

CHE 01

Amefichua kazi hizo baadhi ni kupika na kufua, akibainisha kwamba anachotakiwa mwanamke ni kupata raha na kumshauri mwanaume wake katika mambo mengine huku akisema mwanamume anapaswa kuzifanya kazi za ndani akiwa na mke ama mpenzi wake.

“Mimi kwenye ndoa nina miaka 17 na mke wangu, nafanya shughuli hizo za kupika na kufua, naweza kusema ni moja ya ushindi wa kuishi muda mrefu kwenye ndoa hii, nampenda sana mke wangu. 

“Wala sijarongwa, maana watu wakiona unamsaidia kazi za nyumbani mke wako, basi wanaanza kusema umerogwa, kumbe ni ujanja wa mapenzi tu wa kudumisha ndoa kwa muda mrefu. Kitu kingine ninachoshukuru mke wangu ni mvumilivu sana wa kila kitu,” amesema.

Dk Cheni aliwahi kutamba kwenye maigizo akiwa na Kaole Sanaa Group na tamthilia za kundi hilo zikirushwa kwenye kituo cha runinga ITV.

Kwa sasa mbali na uigizaji wa filamu, anajihusisha na ushereheshaji (MC) na anakiri huko anapata pesa nyingi zaidi kuliko filamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *