Pamoja na hatua hiyo, timu za misaada za Umoja wa Mataifa zimeonya kuwa watoto wengi wa Kipalestina katika eneo hilo hawako katika hali ya kustahimili msimu mwingine mkali wa baridi.

“Tuna matumaini makubwa kwamba mipango ya amani itaboresha hali,” msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Ricardo Pires, amesema alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Geneva leo. “Hata hivyo, hali halisi kwa watoto na vijana huko Gaza inaendelea kuwa ya kutisha sana.”

“Bado tuko katika mawazo ya nadharia,” amesema msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu misaada ya Dharura na OCHA, Jens Laerke, kuhusu azimio la Baraza la Usalama la mpango wa amani wa Marekani, akisisitiza kwamba “linahitaji utekelezaji zaidi”, lakini amekumbusha uungwaji mkono wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maendeleo hayo.

Azimio linaloidhinisha “Mpango Kamili wa Kukomesha Mzozo wa Gaza” uliotangazwa na Rais wa Marekani Trump mnamo tarehe 29 Septemba, lilipata uungwaji mkono kutoka kwa nchi 13 katika Baraza la Usalama. China na Urusi hazikupiga kura.

Bodi ya amani

Azimio hilo linaunga mkono utawala wa mpito unaojulikana kama “Bodi ya Amani” ambayo inaripotiwa kuwa Rais Donald Trump ataongoza ili kuanzisha kikosi cha muda cha kimataifa huko Gaza na kuratibu juhudi za ujenzi upya ikiwemo utoaji wa msaada wa kibinadamu.

Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wake jana usiku, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehimiza kuheshimiwa kwa usitishaji vita na pande zote zinazopigana, ambayo yalisababishwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

Bwana Guterres ametambua “juhudi zinazoendelea za kidiplomasia za Misri, Qatar, Uturuki, Marekani na nchi jirani za kikanda kuhusu mgogoro wa Gaza, kabla ya kusisitiza umuhimu wa kusonga mbele kuelekea awamu ya pili ya Mpango wa Marekani, unaopelekea mchakato wa kisiasa kwa ajili ya kufikia suluhisho la nchi mbili, kulingana na maazimio ya awali ya Umoja wa Mataifa.”

Changamoto zaidi za kibinadamu

Wakati huo huo huko Gaza, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yamesema leo kwamba zaidi ya miaka miwili ya vita vya uharibifu kati ya wapiganaji wa Hamas na Israel na ukosefu wa kudumu wa kila aina ya msaada vimewaacha watu wa eneo hilo wamechoka kabisa.

Katika siku za hivi karibuni, mvua kubwa imejaza maji mahema yaliyochakaa yanazowahifadhi watu waliokimbia makazi yao mara kadhaa kutokana na vita, amesema Ricardo Pires, kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

“Tunashuhudia hadithi za kusikitisha za familia zenye kukata tamaa zinazohisi kupotea kabisa na kuchoka baada ya mahema yao kujaa maji,” amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva. “Watoto wanapolala katika mahema yaliyojaa maji bila mavazi ya joto au matandiko makavu, wengi wakiwa hawana lishe inayohitajika, wakiwa na kinga ya mwili ndogo sana na tayari wameathiriwa kisaikolojia na mzozo, msimu wa baridi unakuwa hatari sana.”

Bwana Pires amebainisha kuwa hali mbaya ya hewa ya hivi karibuni huko Gaza imesababisha ongezeko la watu wanaotafuta msaada wa kimatibabu hasa miongoni mwa watoto waliodhoofishwa na “miaka ya utapiamlo, njaa, kiwewe na kukimbia makazi mara kadhaa.”

Watu huko Gaza wanapita kwenye dimbwi la maji kufuatia mvua kubwa.

© WFP/Maxime Le Lijour

Watu huko Gaza wanapita kwenye dimbwi la maji kufuatia mvua kubwa.

Afisa huyo wa UNICEF pia ameeleza kuwa kwa sababu vikosi vya Israeli vinakalia zaidi ya asilimia 50 ya eneo hilo, maeneo mengi ambayo Wapalestina wamelazimishwa kutafuta hifadhi yako pwani na yana uwezekano mkubwa wa kujaa mafuriko.

Kuongezeka kwa msaada wa kibinadamu kivuko cha Zikim

Katika wito wa kupata msaada zaidi, amesisitiza kuwa hii ilikuwa “sehemu ya mpango wa amani na tunahitaji kuona korido za kibinadamu zikifunguliwa zaidi.”

Kulingana na OCHA, zaidi ya tani 5,400 za misaada zilikusanywa kati ya Alhamisi na Jumapili, ikiwa ni pamoja na malazi, matibabu na vyakula.

Kivuko cha mpaka cha Zikim kimefunguliwa tena baada ya kufungwa kwa miezi miwili, na kufanya idadi ya vivuko vinavyopatikana kuwa vitatu.

Bwana Pires amesisitiza umuhimu wa kufunguliwa kwa kivuko cha Zikim na kusema kuwa hivi karibuni UNICEF ilifanikiwa kuleta makasha 96 ya biskuti za kuongeza nguvu zilizokusudiwa kupelekwa kaskazini mwa Gaza eneo lililokumbwa na njaa.

“Tunahitaji msaada zaidi, mahitaji ni mengi zaidi,” amesema. “Tunatumaini na mpango mpya, hilo litakuwa jambo halisi muhinu kwa watoto na familia”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *