Shinyanga. Wawakilishi wa wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga wamelalamikia wingi wa tozo kwenye huduma moja kutoka halmashauri, sambamba na wazabuni kutolipwa fedha za nyuma wanazodai.
Wakizungumza leo Novemba 18, 2025 katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, wafanyabiashara hao wameeleza uwepo wa risiti bandia za malipo huku halmashauri ikikanusha madai hayo.
“Hatuoni risiti au namba ya malipo ya kodi ya huduma ‘service levy’ kama ilivyo malipo ya mrabaha, lakini tunalipa tena na ushuru wa mashine ya kuvunja mawe ya dhahabu ‘karasha’ ambayo ni sawa na ‘service levy’ bado risiti inaandikwa ya mnada.
“Kwa nini isiandikwe risiti ya karasha kwa kile tunacholipia? Tunaomba halmashauri itupunguzie tozo,” amesema Egina Joyce.
Mwenyekiti wa chemba ya biashara viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama akizungumza katika kikao kazi.
Ameongeza kuwa: “Kuna risiti ambazo si halali zinatolewa kama za malipo, ninaongea kile nilichokishuhudia wala siumbi maneno pia, hata kikao cha awali tulichokaa alikuwepo mkurugenzi aliyetoka sikukubaliana na hili suala ni kama limewekwa kwa nguvu bila sisi kuridhia.”
Naye Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Isack Mwaipopo ameeleza kuwa walijadiliana kuhusu ushuru wa karasha na wafanyabiashara wakakubaliana nao, amekanusha uwepo wa risiti bandia/zisizo halali akidai zote zinazotolewa ni halali.
“Huu ushuru wa karasha tulikaa kikao na wafanyabiashara wa madini wakakubali kulipa, ndio maana tukaweka. Pia, hakuna risiti zisizo halali ambazo zinatolewa kwa wafanyabiashara,” amesema Mwaipopo.
Mwakilishi wa wazabuni kutoka Wilaya ya Kahama, Charles Machali ameeleza kuwa kuna madeni ya nyuma ambayo wazabuni wanazungushwa kukamilishiwa malipo yao, hivyo kusababisha kudorora kwa mitaji.
“Ukiachana na mfumo wa sasa wa ‘force account’ kuna madeni ya zamani ambayo bado hatujalipwa kuanzia mwaka 2014 hadi 2017, tukipeleka hoja kwa tunaowadai wanakubali kulipa lakini malipo hawafanyi.”
“Tunadaiwa kwenye benki, wenyewe hawajali kama unadai halmashauri, wanahitaji rejesho lao na pia sisi tunahitaji kulinda mitaji yetu,” amesema Machali.
Aidha, Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga, Jonathani Manyama ametoa wito kwa halmashauri kuhakikisha madeni ya nyuma yanalipwa kabla ya kikao kijacho.
Pia, ameitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, chini ya katibu tawala, ifuatilie hatua kwa hatua kuhusiana na ushuru wa karasha na maazimio yake,
“Tunatamani kikao kijacho tuwe na kitu kipya na madeni yote ambayo wazabuni wanadai yawe yamelipwa pia, nitoe maagizo ya ufuatiliaji wa maazimio ya kikao cha awali kuhusiana na ushuru wa karasha hatua kwa hatua hadi utekelezaji wake, pamoja na halmashauri kufuatilia uwepo wa risiti zisizo halali zinazodaiwa kutolewa kwa wafanyabiashara,” amesema Manyama.