Dar es Salaam. Baada ya Mousa Camara kufanyiwa upasuaji wa goti juzi huko Morocco, kipa anayeshika nafasi yake kwa sasa, Yakoub Suleiman ametegua mtego wa kwanza kati ya miwili ambayo anatakiwa aikwepe katika kipindi ambacho mwenzake atakuwa anauguza majeraha.

Mtego ambao Yakoub ameushinda hivi sasa, ni wa adhabu ya kukosa mechi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya kufanikiwa kujilinda kutopata mjumuisho wa kadi za njano katika mechi mbili zilizopita ambao ungemuweka katika hatari ya kukosa mchezo mmoja kati ya miwili ya hatua ya makundi ambayo Simba itacheza katika kipindi ambacho Camara atakuwa nje ya Uwanja.

Katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambazo Yakoub alicheza, kipa huyo alimaliza bila kuonyeshwa kadi ya njano, jambo linalompa uhakika wa kucheza mechi mbili zijazo dhidi ya Petro Luanda na Stade Malien.

Kwa mujibu wa kanuni ya 5(i) ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, mchezaji atakosa mchezo unaofuata baada ya kutimiza kadi tatu za njano.

“Mchezaji anayefikisha kadi ya njano ya tatu, atasimamishwa moja kwa moja kucheza katika mechi inayofuata ya mashindano ya Klabu ya CAF. Sekretarieti inapaswa kuwawasiliana na Chama husika juu ya kusimamishwa huko,” inafafanua kanuni hiyo.

Kama Yakoub angeonyeshwa kadi za njano mbili kwenye mechi hizo za nyuma, maana yake kadi ya njano katika mechi inayofuata dhidi ya Petro Luanda ingemkosesha mchezo dhidi ya Stade Malien na hivyo ingeifanya Simba kubaki na kipa mmoja tu mwenye angalau uzoefu ambaye ni Hussein Abel.

Ukiondoa hilo, Simba na Yakoub mwenyewe wanapaswa kuombea kipa huyo aruke kiunzi cha majeraha ili mzigo wa kulinda lango la timu hiyo usibakie kwa Abel pekee ambaye amekuwa hatumiki kikosini kwa muda mrefu.

Kipa wa zamani wa Simba, Iddi Pazi amesema kuwa anaamini Yakoub atalilinda vyema lango la Simba katika mechi atakazokaa langoni kipindi ambacho Camara hatokuwepo.

“Ni kipa mzuri watu wawe na imani naye tu. Hizi timu kubwa zina presha lakini ndani ya muda mfupi anaonekana ameweza kukabiliana nayo. Watu hawapaswi kuwa na wasiwasi naye na naamini atafanya vizuri tu,” alisema Pazi.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said alisema, “michuano mikubwa anayokwenda kucheza isimfanye apate presha, anatakiwa acheze kama anavyocheza mechi za kawaida, hapo ataona matokeo.

“Yakoub anatakiwa acheze kwa kujiamini, akiwaza kwamba yuko pekee yake anaweza kujihurumia na kujikuta anaruhusu mabao kizembe. Simba iko mikononi mwake hivyo mashabiki tunaamini kwenye uwezo wake ambao unatakiwa kudhihirika katika michuano hiyo.”

Mchambuzi wa Soka na kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Amri Kiemba alisema Yakoub anatakiwa kujiamini na kuhakikisha anaifanikisha timu hatua ya makundi, kwani yeye ndie tegemeo.

“Sasa Camara hayupo anaweza kufaa kabisa kuwa mrithi wa Manula, kwani ni mzawa na anapata nafasi kubwa kama hiyo.

“Hizo ni mechi ambazo si Simba tu wanazitazama ila nchi nyingi, hivyo kwangu naona ni wakati wake wa kuonyesha ubora,” alisema Kiemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *