
Urusi imeikabidhi Ukraine, siku ya Alhamisi, Novemba 20, miili 1,000, iliyowasilishwa kama ile ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa vitani, idara ya Ukraine inayosimamia wafungwa wa vita imetangaza.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Leo, hatua za kurudisha miili makwao zimefanyika. Miili elfu moja, iliyowasilishwa na upande wa Urusi kama ile ya wanajeshi wa Ukraine, imerejeshwa nchini Ukraine,” Kituo cha Wafungwa wa Vita cha serikali ya Ukraine kimesema kwenye Telegram.
Utambuzi wa miili iliyorejeshwa utafanywa “hivi karibuni” na wachunguzi na wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, imeongeza.
Zoezi la mwisho la kurejesha miili ya wanajeshi waliouawa lifanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba na pia lilihusisha miili 1,000.
Zoezi hili la hivi karibuni lnaleta idadi ya miili iliyorejeshwa na Urusi nchini Ukraine tangu mwanzo wa mwaka hadi zaidi ya 15,000. Ukraine, kwa upande wake, imerejesha miili mia kadhaa nchini Urusi katika kipindi hicho.
Ubadilishanaji wa miili ya wanajeshi waliouawa na wafungwa wa vita ndio matokeo pekee ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili zinazopambana, zaidi ya miaka mitatu na nusu baada ya kuanza kwa mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine.
Februari iliyopita, Rais Volodymyr Zelensky akiambia kituo kimoja cha televisheni cha Marekani kwamba nchi yake imepoteza karibu wanajeshi 46,000 tangu mwaka 2022, takwimu ambayo wachambuzi wanaiona kuwa ya chini sana, huku “makumi ya maelfu” ya wengine wakiwa wamepotea au wamechukuliwa mateka na jeshi la Urusi.