
Kwanza, nampongeza Rais Samia Suluhu kwa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake ya Novemba 14, 2025 alipohutubia Bunge la 13, akisema amehuzunishwa na matukio hayo na kwamba angeunda tume kuchunguza.
Alisema katika siku tajwa, baadhi ya watu walipoteza maisha, wengine walipoteza mali na miundombinu ya umma imeharibiwa na kuchomwa moto.
Mkuu huyo wa nchi alisema ripoti ya tume hiyo, itaiongoza Serikali kuanza mchakato wa maridhiano kupitia Tume ya Maridhiano na Upatanishi itakayoiunda hapo baadaye.
Wajumbe walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.
Katika tume hiyo, pia yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Ukiangalia wanaounda tume hiyo ni majina makubwa ya viongozi wazoefu katika maeneo mbalimbali, wamehudumu taasisi kubwa ndani na nje ya nchi.
Japo hadidu za rejea hazijawekwa wazi lakini ni wazi kuwa hiyo ni hatua nzuri ya kupongezwa, kwani inaonyesha kujali na kutafuta suluhisho.
Hata hivyo, kwa kuwa sina uhakika kama nitapata nafasi ya kutoa maoni katika tume hiyo, nitadokeza machache ambayo pengine yanaweza kusaidia uchunguzi huo, kwanza niseme mimi si mtaalamu wa masuala ya uchunguzi wa matukio ya kiusalama, isipokuwa mimi ni mwandishi wa habari tu.
Tofauti na watu wengi wanavyoweza kuhusianisha vurugu zilizotokea na mambo mbalimbali, kwa mtazamo wangu suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, ni changamoto kubwa iliyochangia hali iliyojitokeza.
Vijana wengi wa Kitanzania wapo mtaani bila shughuli mahususi za kufanya licha ya kuwa wengi wao ni wasomi, wana ujuzi mbalimbali lakini pia wana nguvu na akili za kutumika katika maeneo tofauti. Mtu asiye na shughuli mahususi za kufanya ni rahisi kupata ghadhabu na kuungana na walioghadhabika.
Na ndiyo maana wakati wa vurugu hizo kulikuwa na kundi kubwa lililokuwa likiiba na kupora mali za watu. Hata hivyo, wizi na uporaji ni tabia binafsi ambayo wakati mwingine inaweza isiwe na msukumo wowote.
Lakini pia msukumo wa kisiasa japo si kwa ukubwa, una mchango wake katika yaliyotokea, raia wengi ni kama walikuwa na hasira ya muda mrefu dhidi ya kundi fulani na walipopata fursa wakaionyesha, ndiyo maana mali zilizoharibiwa ni za makundi fulani mahususi karibu kila kona.
Kwa upande wa maisha yaliyopotea idadi kamili bado haijafahamika lakini kwa sauti za vilio vinavyosikika kila kona ni dhahiri kuwa maisha ya watu wengi yamepotea. Hili ni jambo la kuhuzunisha, hata mkuu wa nchi ameomboleza maisha yao.
Nini ambacho kimesababisha kupotea kwa maisha ya watu wengi, mosi ni wananchi kutokutii amri zilizotolewa na vyombo vya usalama baada ya kutoa amri ya watu kutotoka nje baada ya saa 12 jioni ya Oktoba 29, hii ni kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Hata ukisikia vilio vya wengi ni kama maisha yalipotea zaidi Oktoba 30, kwa nini?
Pengine vyombo vya ulinzi viliamini ambaye amekaidi na kutoka nje ni mwandamanaji ambaye amedhamiria kukabiliana navyo, ingawa mamlaka zilisahau kuwa marufuku ya kijeshi ilikuwa ni msamiati mpya nchini Tanzania.
Kwa mataifa yaliyozoea vurugu kila mmoja angeelewa tangazo lile lilimaanisha nini lakini katika kisiwa hiki cha amani wengi walidhani ni kutokwenda barabara kubwa, busara ingeweza kutumika katika mtazamo wa watu kutojua maana ya tangazo kwa kuwa hawakupata hata fursa ya kufafanuliwa.
Watembeaji baada ya marufuku bila shaka hawakuwa na silaha, hivyo wengeweza kudhibitiwa kwa namna nyingine na si matumizi ya nguvu kubwa.
Lakini pia kutokana na juhudi za Serikali kuiweka dijitali mbele hivi sasa wengi wanapata habari na taarifa kwa mtandao, wakati marufuku inatolewa mitandao ilikuwa imezimwa, hivyo si wote waliipata.
Matangazo yalitolewa kwenye runinga na redio ambavyo vilibaki kama njia ya mawasiliano huku wengi wanasikiliza kwenye gari na si lazima wawe kwenye runinga. Ni bora ungetumwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu kwa sababu idadi ya simu hai ni takribani milioni 100 na hivyo watu wengi wangeupata.
Pia kupitia mtandao na vyombo vya habari nimesikia baadhi ya watu walipigwa na risasi wakiwa nyumbani kwao, kwenye magari na maeneo mengi ambayo walidhani ni salama kwao, hili linahitaji kuchunguzwa kwa kina kwa kuwa naamini watumishi wa vyombo vya ulinzi wanaotumia silaha wanakuwa wanajua uwezo wake. Hayo ndiyo maoni yangu kwa Tume.
Mungu ibariki Tanzania.
Ephrahim Bahemu anapatikana kwa namba 0756939401