
Dar es Salaam. Niliposikia vijana wanapewa wizara yao nimewaza mengi sana. Kwanza nimefurahi kwa sababu vijana wanabeba mengi sana vichwani mwao. Kama binadamu, ni lazima nao wajitegemee na kuanzisha familia kama walivyofanya wazazi wao, lakini watazileaje ilhali hawana kipato?
Afadhali mambo mengine nayo yangesubiri, yaani wangelibaki kuwa watoto mpaka kitakapoeleweka. Lakini kibaiolojia wanakomaa na kuzeeka bila kuwa na njia za kulijenga Taifa lao.
Kila asubuhi unapishana na kijana akiwa na begi mgongoni. Ungeona ndani ya begi hilo kunani, usingeweza kuamini hata kidogo. Vyumba viwili vya begi vimejazwa vyeti vya kuanzia Shule ya Chekechea hadi vyuo vikuu. Chumba cha tatu kina nguo za kubadilisha, maana hajui atalala huko aendako au atarejea. Usione ajabu chumba cha mwisho kikibeba vichupa vya plastiki vilivyobeba pombe kali.
Mzigo wa chumba cha mwisho cha begi lake, unasababishwa na mzigo wa mawazo ulio kichwani mwake. Hii ni ishara kuwa hajui anakwenda kutafuta kazi au kujiliwaza dhidi ya mawazo. Kumbe tayari kijana wetu ameshaathiriwa na msongo wa mawazo.
Hii ni kwa sababu hana mtu anayeweza kumsikiliza na kumwelewa kirahisi. Ndio maana nahisi wakiwa na wizara yao itakayosimamiwa na vijana wenzao, angalau watapata pa kuanzia. Inasemwa kuwa “Ndege wa rangi moja huruka pamoja”.
Tulipokuwa wanafunzi, wazazi wetu walituhadhari sana na ukazi wa vijiweni. Jirani na nyumbani kulikuwa na kijiwe maarufu tulichokiita “Gogovivu”. Kilikuwa ni kipande cha mti ulioangushwa kutoka nyumba ya jirani, tukakivutia chini ya kivuli cha mti mkubwa tulioutambua kwa jina la Mkrismasi. Jina hilo lilitokana na mti huo kuchanua maua mekundu kila uliofika msimu wa mwisho wa mwaka.
Pamoja na kuwasikiliza wazazi, ilikuwa ni lazima vijana wa mtaani tukutane pale kuongelea mambo yetu hata ikiwa kwa siri. Kuna mambo yasingelienda sawa iwapo tungeyakalia kimya. Aibu isingelikwenda kwa wazazi wetu, bali tungeibeba sisi wenyewe.
Lakini kama tungefanikiwa kuyashinda, heshima ingelikuja mtaani. Hata wazazi hawafurahii kuwaona watoto wao wakiishi kama wadumavu. Walifurahi kuona tuking’ara mjini na kusifiwa kokote tulikoenda: “Watoto wa kishua wanaingia”.
Wakati huo tulikuwa na jambo kubwa lililotulazimu kulikalia vikao kila jioni. Timu yetu ilikuwa katika fainali ya ligi ya uswazi. Mchezo wetu wa mwisho ulikuwa baina ya mahasimu wetu wakubwa, Makokoni Shooting Stars.
Uhasimu wetu haukuwa katika ulinganifu wa viwango vya kimpira, bali hawa jamaa walikuwa wababe. Mara zote sisi tulipoibuka washindi dhidi yao, wao walikuwa wakitutisha na silaha zenye ncha kali ili tukubali kushindwa.
Enzi hizo hatukuwa na usajili wala bodi ya ligi. Hivyo jamaa waliweza kumtuliza refarii na kujichukulia ushindi kwa njia za kibabe. Na hatukuweza kujitoa mashindanoni kwa sababu kufanya hivyo ni kukubali kuwa watumwa wao.
Wangeendelea kuja mtaani kwetu na kutunyanyasa pamoja na kutupora senti za matumizi tulizobakiza shuleni. Ingekuwa ni aibu kubwa kwa dada na wenzi wetu wa mtaani, kwani hata wao wangeweza kuporwa mikononi mwetu kwa namna hiyo.
Katika kikao chetu kabla ya mchezo, tuliweka maazimio ya “kufa kishujaa”. Liwalo na liwe, lakini fainali hii ni lazima kieleweke. Siku ya mechi kama kawaida walituoneshesha silaha zao mapema ili tuendelee kuwa wapole. Sisi tulicheza kama wanyonge lakini zilipobaki takribani dakika kumi kabla mpira haujaisha, tukapeana ishara. Tulikuwa tumeshamsuka refarii kuenenda na mpango wetu.
Tulibadilika ghafla na kuwashambulia kama kimbunga, tukiwamwagia mchanga wa uso na kuwatandika bakora. Tukawapiga bao mbili za chap chap, kabla hawajarudisha akili zao refa akamaliza mchezo. Wakati wao wakichomoa silaha zao, wakagundua kuwa nasi tulikuwa na jeshi kubwa na silaha za maangamizi. Kutoka siku hiyo heshima ilichukua mkondo, na sote tukaishi kama watu.
Sasa nafikiria wizara ndio ingekuwa na watoto wa mtaani. Wachukulie kwanza wale waliojikatia tamaa wakaangukia kwenye pombe na kamari. Picha linaanza kwa mmoja kumshauri mkubwa wake: “Mwanangu mi naona “Wizara ya Vijana” kama haijakaa poa. Kwa nini tusiliite “Chama la Wana”? Yaani kama skani flani vile…” Mwingine naye anachangia la moyoni mwake: “Au tuite Jobless Corner? Si unajua wana ndio kwanza tunajitafuta…”
Japo haitakuwa hivyo wizarani, lakini watendaji wa wizara wawe ni vijana wanaoelewa lugha ya wenzao huku mtaani. Kitu kimoja ambacho wengi hawakijui kutoka uswazi, ni kwamba watu wana akili kama mchwa. Mimi nawafananisha na wapiganaji wanapokuwa katika uwanja wa mapambano. Mbinu zinaweza kutumika kinyume lakini zikaleta tija. Ni sawasawa na waraibu wanavyoijua vita dhidi ya dawa za kulevya kuliko wanazuoni.
Hivyo iwapo watendaji wa Wizara ya Vijana wataondoa tofauti kati yao na vijana wenzao, tutegemee kupata suluhisho la matatizo ya vijana. Wazingatie kuwa huku mtaani ndiko ilikolala nguvukazi ya Taifa, inayohitaji kuamshwa na kuwezeshwa.
Bado tuna raslimali ardhi ya kutosha kwa kilimo na viwanda. Ninaamini vijana wanaweza kuelewana kwa lugha yao namna ya kuunganisha raslimali hizi (vijana na ardhi), na Serikali ikatoa mitaji. ili kukuza kwa kasi uchumi wa nchi yetu.