Marekani. Kuwa gerezani siyo mwisho wa malengo, mtandao wa TMZ umenasa picha na video za gwiji wa muziki wa hiphop duniani, Sean Combs maarufu P Diddy akifanya shughuli zake za kawaida akiwa gerezani.
P Diddy alihukumiwa Oktoba 3, jijini New York baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya usafirishaji watu na kushiriki katika ukahaba.
Diddy alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja gerezani. Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 05,2025.
Picha zinaonyesha mkali huyo wa muziki wa Hip Hop akimalizia kazi jioni katika maktaba ya vyombo vya habari ya Fort Dix iliyopo kwenye kanisa ambako husaidia kuwapatia wafungwa filamu na vitabu vya dini kwa ajili ya elimu au kuandaa kazi za kisanii.
P Diddy ambaye kwa sasa nywele zake zimeota mvi anaonekana gerezani akivua skafu na koti la bluu na kubaki na sare yake ya kijivu ya gerezani.
Picha hizo zinaonyesha Diddy akiwa na hisia tofauti wakati mwingine akisononeka na wakati mwingine mwenye furaha na nyingine akiwa amelewa. Diddy anatumikia kifungo cha miezi 50 baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja Sheria ya Mann akitarajiwa kuachiwa 2028.