Dodoma. Takribani siku 10 zimepita tangu ulipotokea msiba wa mshereheshaji na mchekeshaji maarufu, Emmanuel Mathias (MC Pilipili) ambaye Jeshi la Polisi lilitangaza kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida, bado wingu zito limetanda.

Msemaji wa familia ya MC Pilipili, Mchungaji Christopher amesema kuwa hadi leo Jumanne Novemba 25, 2025 hakuna taarifa zozote ambazo zimetolewa na jeshi la Polisi wala chombo kingine chochote kuonyesha kama kuna juhudi au kuna mahali wanamshuku mtu kuhusiana na mauaji hayo.

Mwili wa MC Pilipili ulipelekwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako inasadikiwa kwamba alifikishwa hapo na walioitwa wasamaria wema.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi alisema kuwa, Novemba 16, 2025 saa 11 jioni wasamaria wema waliupeleka mwili wa mshereheshaji huyo na baada ya kuuchunguza walibaini alishapoteza maisha.

“Hadi leo ninazungumza na wewe sisi kama familia hatujapata taarifa zozote kutoka mahali popote zinazohusiana na nini kinaendelea kuhusu kifo cha ndugu yetu huyo, lakini kama wanadamu maumivu tunaendelea kuwa nayo,” amesema Mchungaji Christopher.

Novemba 18,2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera alinukuliwa akisema kifo cha kifo cha Pilipili hakikuwa cha kawaida na kinaonekana kilisababishwa na kupigwa.

Hata hivyo alipotafutwa leo kuzungumzia hatua zilizofikiwa kuhusu uchunguzi hupo mara kadhaa simu yake haikupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe kwenye simu ya mkononi hakujibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *