Marekani. Ngoma ya Justin Bieber inayokwenda kwa jina la Ghost imezua gumzo hivi karibuni kutokana na mashairi yake, baadhi ya mashabiki wakiyafananisha kama alimuimbia aliyewahi kuwa mpenzi wake Selena Gomez.
Wimbo huo ulitoka miaka minne iliyopita lakini umekuwa gumzo mitandaoni hivi karibuni baada ya watu kujua mistari ya wimbo huo.
Machi 19 mwaka huu Justin Bieber aliachia albamu yake ya sita, ‘Justice’ moja ya nyimbo zinazozungumziwa sana kwenye albamu ya Justice ni ‘Ghost’, huku mashabiki wengi wakiwa na nadharia mbalimbali kama mashairi ya wimbo huo yaliandikwa kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani, Selena Gomez.
Kumekuwa na idadi kubwa ya tweets zikijadili kwanini watu wanaamini ‘Ghost’ inamhusu Selena, huku wengine wakipinga wazo hilo.
Hata hivyo Bieber mwenyewe alieleza kuwa wimbo huo unahusu kumpoteza mtu kwa njia ya kihisia au kimwili, mashairi na hisia za wimbo huo zimewafanya mashabiki wahoji kama bado anamisi Selena ambaye kwa sasa ameolewa na Benny Blanco.
“I miss you more than life”. Huu ni mstari ambao mashabiki wameshikilia ukionekana kuakisi hisia nzito ambazo Justin na Selena walipitia katika uhusiano wao wa miaka minane, uhusiano uliokuwa na upendo, pia maumivu mengi.
Wakati mashabiki wakifikiria hilo Justin kwa sasa anaishi maisha mapya na mke wake, Hailey Bieber, ambaye alimuoa mwaka 2018. Amewahi kuandika nyimbo kadhaa kuhusu mapenzi yao katika albamu hiyo hiyo ya Justice.