Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Rayvanny anaendelea kufanya vizuri na wimbo wake mpya, Songi Songi (2025), ukiwa ni toleo jipya kutoka kwenye ule unaokwenda kwa jina hilo, wa Salima Chica ambaye wameshirikiana.
Salima Chica kutokea DR Congo aliachia wimbo huo miezi mitatu iliyopita na kupata mapokezi makubwa, ndipo Rayvanny akaona waurudie (remix) kwa mtindo wa kolabo kama alivyofanya kwa wasanii baadhi.
Toleo la awali limekubalika na wengi, mathalani tayari video yake imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 13 ukiwa ni wimbo wa kwanza kwa Salima Chica kufanya hivyo katika mtandao huo.
Songi Songi Remix (2025), ni wimbo unaovuta hisia za wengi ukichanganya midundo ya Bongofleva na mahadhi ya kusisimua yanayofaa kuchezeka.
Rayvanny kutokea Next Level Music (NLM), ameongeza sauti yake laini na mistari ya kuvutia, na kuupa wimbo huo ladha mpya na yenye kuvutia ambayo inasherehekea mapenzi, furaha na maisha ya mtaani.
Hata hivyo, kabla ya Salima Chica, tayari Rayvanny alishafanya remix za nyimbo za wasanii wengine kutoka Bongo na hata kimataifa kama ifuatavyo.
1. Rosa Ree
Mshindi huyu wa tuzo tano za Hip Hip, alipoachia wimbo, Sukuma Ndinga (2020) na kufanya vizuri, moja kwa moja Rayvanny alimuomba remix. Rosa alikubali na hadi sasa video yake imetazamwa YouTube mara milioni 2.
“Unajua kolabo tunafanya kutokana na vibe na muziki unatakiwa ufanye muda huo kutokana na kitu ambacho umekifurahia. Kwa hiyo Rayvanny alisikia wimbo huo akaupenda sana, akanipigia simu tufanye kitu,” anasema Rosa Ree.
Rosa Ree aliyetoka na ngoma, Up In The Air (2017) chini ya The Industry, alisema kitendo cha wimbo huo kuwekwa katika chaneli ya Rayvanny YouTube, ni makubaliano ya menejimenti za pande zote mbili.
Tayari Guchi kutokea Nigeria alikuwa imeishika Afrika na wimbo wake, Jennifer (2021), Rayvanny alipousikia akavutiwa nao, ndipo akamwalika Guchi Bongo ambapo walirekodi remix pamoja na kushuti video yake.
Hadi sasa Jennifer Remix (2021), ni moja kati ya nyimbo chache za Guchi zenye mafanikio makubwa ukiwa umetazamwa YouTube (chaneli ya Rayvanny) zaidi ya mara milioni 27.
3. Mavokali
Kipindi kifupi baada ya Mavokali kuachia wimbo wake, Mapopo (2022), ulifanya vizuri kimataifa na hata kuzizidi nyimbo nyingi za wasanii wakubwa Bongo kwa wakati huo ambapo walijiuliza dogo amewezaje!.
Basi Rayvanny akaona hiyo ni fursa na ndipo akarekodi remix ila Mavokali akawa mjanja kwa kuweka video hiyo katika chaneli yake tofauti na wasanii wenzake na tayari imetazamwa mara milioni 22 huko YouTube.
4. Lil Jay Bingerack
Ni staa wa muziki kutokea Ivory Coast ambaye aliwakosha wengi Afrika kupitia wimbo wake, Hi Hi Hi (2023), basi Rayvanny akaona hiyo ni nafasi ya yeye kupenya zaidi ukanda wa Afrika Magharibi.
Mara moja wakaingia studio na kurekodi remix yake ambayo video yake hadi sasa imetazamwa YouTube mara milioni 1.3, huku ikiwekwa pia katika chaneli ya Rayvanny, mshindi wa tuzo ya BET 2017.
5. Chino Kidd
Kuna kipindi upepo wa muziki ulikuwa upande wa Chino Kidd, kila wimbo aliyotoa ulipata mapokezi mazuri, na mmoja wapo ni Kibela (2023) akiwa na Mfana Kah Gogo na S2kizzy ambaye ni mtayarishaji wake pia.
Kama kawaida Rayvanny akaomba remix na kuwashirikisha wote waliokuwapo katikaa toleo la mwanzo, huku video akiiweka katika chaneli yake na hadi sasa huko YouTube imetazamwa mara milioni 3.4.
6. Misso Misondo
DJ huyu na kundi lake la Wazee wa Makoti, walikuja kwa mtindo wa tofauti wa kupiga na kuucheza muziki wa Singeli, na ndani ya muda mfupi wakajizolea mashabiki wengi ndani na nje.
Mara moja Rayvanny akafanya remix ya wimbo wao, Kitu Kizito (2023) akiwashirikisha, ulifanya vizuri hadi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Singeli 2023. Na video yake imetazamwa mara milioni 7.1 katika chaneli ya Rayvanny.
Akiwa anaendelea kuijenga chapa yake katika Bongofleva, Dayoo alikuja na ngoma yake, Huu Mwaka (2024) ambayo ilibamba sana na kulipasha jina lake kutokana na ubunifu wa kipekee aliokuja nao.
Kwa mujibu wa Dayoo akaona kuna haja ya kufanya remix na ndipo akamuomba Rayvanny ambaye alikubali. Kazi ikafanyika na hadi sasa video yake imetazamwa mara milioni 16.
“Makubaliano yote kati yetu yapo kwenye mikataba. Vitu vipo kwenye mikataba tayari kwa maslahi ya pande zote mbili,” anasema Dayoo kuhusu video hiyo kuwekwa katika chaneli ya Rayvanny huko YouTube.
Hivyo upande huo wa kufanyia remix nyimbo za wasanii wengine, kwa Rayvanny upo kibiashara zaidi maana kwa sehemu kubwa gharama huzibeba yeye, na ndio sababu kazi hizo anaziweka katika chaneli yake.